Habari za Punde

Wananchi mji mkongwe wapendekeza serikali nne tume ya katiba

Na Editha Majura

WAKATI idadi kubwa ya wakazi wa Jimbo la Mji Mkongwe kisiwani Unguja wakidai serikali ya Zanzibar na Tanganyika zenye mamlaka kamili ndani na nje ya nchi, wawili kati ya wananchi hao wamekwenda mbali zaidi na kudai kuwe na Serikali nne, ya Unguja, Pemba, Tanganyika ndipo Serikali hizo ziunde Serikali ya Muungano kwa namna itakavyoonekana inafaa.

Agnes John (29) mkazi wa Shehiya ya Mkunazini akizungumza mbele ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwenye mkutano wa kuchukua maoni ya wananchi uliyofanyika kwenye Shehiya ya Shangani alisema, “mimi naona ili watu tuwe huru na kudumisha amani, Serikali ziwe nne; yaani Serikali ya Tanganyika, Unguja, Pemba na baada ya kupatikana Serikali hizo ndipo ziamue zitaungana katika maeneo gani.

Naye Kalunde Martin Mrkdonardi {24} alizungumza mbele ya wajumbe hao kuwa anataka Serikali nne, yaani Serikali ya Unguja, Pemba, Tanganyika na ile ya Muungano kwa maelezo kwamba kwa njia hiyo, muungano utakaopatikana utakuwa wa haki na wenye usawa.

Ally Salehe Suleyman {55} alisema anataka muungano wenye mfumo wa Serikali mbili zenye mamlaka kamili, Rais wa Zanzibar awe mtendaji, nchi hiyo iwe na mabalozi katika nchi zote zitakazoonekana zinafaa na wananchi wawe na uwezo wa kumpigia kura ya kumwondoa madarakani kiongozi aliyepata wadhifa kwa kupigia kura na wananchi, ikionekana utendaji wake haunufaishi wananchi.

Mbali na madai ya Serikali kamili za Zanzibar na Tanganyika kutawala mkutano huo, maoni mengine yaliyochukua nafasi kubwa ni yaliyotaka mfumo wa elimu ya awali mpaka kidato cha sita unaotumika visiwani humo uwe sawa na Tanzania bara, ikiwa hilo haliwezekani, ilielezwa na Fadhia Saleh mkazi wa mjini Magharibi kuwa kila nchi iheshimu mtalaa wa elimu wa nchi nyingine pale wahitimu wao wanapokutana katika vyuo vikuu.

Unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto na wanawake pia ni miongoni mwa maoni yaliyochukua nafasi mkutanoni ambapo Fatma Hamza Rajab (61) mkazi wa Shehiya ya Shangani alisema kwa mujibu wa taarifa rasmi alizonazo, kwa kila siku, wastani wa watoto watano wanabakwa visiwani humo hali aliyoeleza kuwa ni mbaya na akataka Katiba ijayo iweke mazingira mazuri ya kukubali kutumika ushahidi hata wa mazingira ili kudhibiti vitendo hivyo dhalimu.

Naye Ibrahim Hassan Ahmed alitaka Zanzibar kuwa na uwezo wa kuwapatia wananchi wake vibali vya kusafiri (Passport), sarafu yake, irejeshewe kiti chake katika Umoja wa Mataifa (United Nations) na kwamba miaka (arobaini na nane) inatosha kuvumilia muungano ambao aliuita wa kinyonyaji
 
Chanzo: Mwananchi

1 comment:

  1. Hakuna kitu kibaya kama watu kukosa elimu..yaani watu wanapata nafasi adhimu kama hii halafu wanaichezea?

    ..Eti serikali nne!..eti..Z'bar iwe na sarafu yake na kiti umoja wa mataifa..!

    Kuna vitu hapa ni very 'basic' watu wanatakiwa wavizungumzie ikiwa ni pamoja na wabunge kuwa na 'university Degrees' pamoja na kuwa na mfumo wa pamoja wa kuteuwa wakuu wa mikoa na wilaya kati ya Bara na Z'bar na mmoja kuweza kufanya kufanya kazi popote ktk jamuhuri.. hawa wa kwetu wamezidi kuwa 'vimeo'

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.