HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA
RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI
KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA KUMI WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR,
TAREHE 29 JANUARI, 2013
TAREHE 29 JANUARI, 2013
1. Mheshimiwa Spika,
nianze hotuba yangu hii kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwingi wa
Rehema, kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana katika Mkutano huu wa
Kumi wa Baraza la Wawakilishi, mkutano ambao umefanyika kwa maelewano makubwa
sana. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuiweka nchi yetu katika hali
ya amani, salama na utulivu na kutuwezesha kupiga hatua kubwa za kimaendeleo ya
kijamii na kiuchumi.
2. Mheshimiwa
Spika,
nakupongeza kwa dhati wewe Mwenyewe pamoja na wasaidizi wako wakuu, ambao ni
Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza kwa kuendelea kuliongoza Baraza letu kwa
busara, hekima, umakini, na ufanisi mkubwa na kufuata vyema misingi ya
kidemokrasia na Kanuni za Baraza. Nachukua fursa hii pia kuwapongeza Wenyeviti
na Wajumbe wa Kamati mbali mbali za kudumu za Baraza kwa kutekeleza majukumu
yao kwa hekima kubwa, na kwa haki na uadilifu lengo likiwa kuliwezesha Baraza
lako Tukufu kutekeleza majukumu yake ya kusimamia shughuli za Serikali na kuona
kwamba shughuli hizo zinaendeshwa vizuri na kwa uadilifu.
3. Mheshimiwa Spika, kwa aina ya kipekee, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa kuendelea kuiongoza nchi yetu kwa umakini mkubwa, hekima, busara
na uadilifu. Uongozi wa Mheshimiwa Rais
ndio chachu ya maendeleo tunayoendelea kuyapata katika nyanja za kijamii na
kiuchumi. Sote ni mashahidi jinsi Rais
Shein anavyoonyesha kwa vitendo utendaji bora katika Serikali na kuhimiza
watendaji kubadilika na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea, ingawa
bado kwa baadhi ya watendaji tabia hii inawapa taabu kuiacha. Nawaomba sana waiache tabia hiyo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na
tunamuomba Mwenyezi Mungu amzidishie hekima, afya njema na uwezo wa kuiongoza
nchi yetu. Amin.
4.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza
sana Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa
kumsaidia vizuri Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa mashirikiano makubwa anayompa katika kuiendesha nchi yetu. Natoa shukrani nyingi kwa Wajumbe wote wa
Baraza la Wawakilishi kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao ya msingi ya
kuwasilisha mawazo ya wananchi waliowachagua na pia kwa kusimamia vyema
utendaji wa Serikali yetu ili kuona utendaji bora wa Serikali katika kukuza
uchumi wa nchi na kutoa huduma kwa jamii ya Wazanzibari. Vile vile, nawapongeza sana Mawaziri, Naibu
Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na Watendaji wote
wa Serikali kwa kuendelea kuchapa kazi na kuiletea maendeleo nchi yetu.
5. Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuvipongeza na kuvishukuru Vyombo vya Habari vyote hapa Zanzibar, hasa Shirika la
Habari la Zanzibar (ZBC) kupitia Redio na Televisheni ambavyo viliendelea
kurusha moja kwa moja maendeleo ya shughuli za Baraza yalivyokuwa yanakwenda na
kuwawezesha wananchi wetu kufuatilia kwa makini hoja, michango na mijadala
iliyoendeshwa Barazani. Kwa furaha kubwa nawapongeza na kuwashukuru wakalimani
wa lugha ya alama kwa kazi zao nzuri walizozifanya kutafsiri mijadala kwa
ishara ili wananchi wetu wenye ulemavu wa kutokusikia, nao waweze kufuatilia
mijadala ya Baraza.
MASUALA MUHIMU YALIYOJIRI NCHINI:
6.
Mheshimiwa Spika, kama sote tunavyoelewa nchi yetu imo
katika harakati za mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tume ya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba tayari imemaliza kazi yake ya kukusanya
maoni kutoka kwa wananchi na Taasisi mbali mbali hapa Zanzibar na Tanzania Bara
na pia imeshakamilisha zoezi hilo kwa upande wa Viongozi. Nachukua fursa hii
kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi wote Unguja na Pemba kwa kujitokeza
kwa wingi kutoa maoni yao. Sasa ni kazi ya Tume kufanya uchambuzi wa maoni ya
wananchi na naamini kabisa kwa uwezo wa Wajumbe wa Tume hiyo nchi yetu itapata
Katiba mpya yenye kukidhi matakwa ya wananchi walio wengi na ambayo itaendeleza
umoja na mshikamano wetu na kudumisha muungano wa nchi yetu. Wakati Tume
inaendelea na kazi zake za kuandaa rasimu ya Katiba, nawasihi wananchi wote
tuwe wastahamilivu na tuendelee kuchapa kazi ili tuweze kuiletea nchi yetu
maendeleo kwa faida ya wananchi wetu na kwa faida ya vizazi vyetu vijavyo.
7.
Mheshimiwa Spika, katika mwezi wa Agosti, 2012 nchi yetu
ilikuwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi, zoezi ambalo limefanyika kwa
mafanikio makubwa licha ya kujitokeza changamoto katika baadhi ya maeneo. Matokeo
ya Awali ya Sensa hiyo yalitangazwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 31 Disemba, 2012 katika viwanja vya Mnazi
Mmoja Dar es Salaam. Matokeo
hayo yanaonyesha kwamba Tanzania hivi sasa tupo watu 44,929,012 na Zanzibar
tumefikia watu 1,303,560. Kwa upande wa
Zanzibar, idadi hii ya watu ni kubwa na kwa kweli tunahitaji kuwa na mipango
madhubuti ya kudhibiti ongezeko la kasi la idadi ya watu. Sasa inatulazimu kuongeza bidii katika
kufanya kazi na kuzalisha kwa wingi bidhaa zitakazokidhi mahitaji yetu ya ndani
na kupata ziada ya kuuza nje. Vile vile, tutahitajika kuimarisha huduma za
jamii, ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama na makaazi.
Nawasihi Viongozi wote katika ngazi zote na
wananchi kwa ujumla tuzidishe mashirikiano na tuzidishe ari ya kujituma
na kuwajibika zaidi katika maeneo yetu ya kazi katika sekta ya umma na sekta
binafsi.
8. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sensa ya 2002, Zanzibar
ilikuwa na watu wapatao 980,000. Katika
Sensa ya 2012, miaka kumi baadae, Zanzibar inayo watu 1,303,560. Ongezeko la watu 323,560. Hili ni ongezeko kubwa sana. Hatuna budi sasa tufanye maarifa ya kupunguza
kasi ya kuzaliana ili watoto wetu tuwalee vizuri zaidi.
9. Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Januari, 2013, nchi
yetu iliadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Katika
maadhimisho hayo, miradi 53 ya maendeleo iliwekewa mawe ya msingi na
kuzinduliwa. Miradi hiyo inathamani ya wastani wa Shilingi bilioni 97 na
ilikuwa katika sekta ya elimu, maji safi na salama, afya, kilimo, uvuvi na
miundombinu ya habari, mawasiliano na barabara. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo
ambayo nchi yetu imepiga katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Nachukua
nafasi hii kuwashukuru kwa dhati Viongozi katika ngazi zote na wananchi wote
kwa kushirikiana katika kufanikisha sherehe zetu hizi adhimu ambazo zilifana
sana.
10.
Vile
vile, nawashukuru makamanda na askari wa vikosi vyetu vya ulinzi, Wajumbe wa
Kamati ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho na Wanafunzi walioshiriki
katika halaiki na maandamano na Wanahabari kwa kazi nzuri waliyoifanya ambayo
imetuletea mafanikio makubwa katika maadhimisho ya Mapinduzi yetu. Hivi sasa tunakabiliwa na maandalizi ya
maadhimisho ya Mapinduzi ya kutimiza miaka 50 (nusu karne) ifikapo tarehe 12
Januari, 2014. Ni imani yangu viongozi sote na wananchi tutaendelea
kushirikiana ili kuzifanya sherehe zetu hizo kuwa za mfano na za hadhi ya juu
kulingana na umuhimu na hadhi ya Mapinduzi yetu.
11.
Mheshimiwa
Spika, hivi
karibuni nilipata fursa ya kuzindua utekelezaji wa Mradi wa TASAF Awamu ya Tatu
hapa Zanzibar. Mradi huu unatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar na una jumla ya
Shilingi Bilioni 470 ambazo zitatumika kusaidia kaya masikini kwa kipindi cha
miaka mitano (5) ijayo. Naomba niwaelekeze watendaji wote watakaohusika na
utekelezaji wa mradi huu kufanya kazi kwa makini, bidii na uadilifu ili
kuhakikisha malengo na matarajio ya mradi huu yanafikiwa. Viongozi kwa upande
wao hawana budi kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki kikamilifu
katika utekelezaji wa mradi huu, ikiwa ni pamoja na kubuni miradi mbali mbali
itakayokuwa na manufaa kwao.
12.
Mheshimiwa
Spika,
lengo la Serikali zetu kuandaa mradi huu ni kutekeleza kwa vitendo ahadi zake
kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 ya kuwawezesha wananchi
kiuchumi na kupunguza makali ya umasikini. Nachukua nafasi hii kuwapongeza sana
wananchi wa Unguja na Pemba na viongozi na watendaji wote walioshiriki katika
utekelezaji wa TASAF Awamu ya Pili kwa kazi nzuri walizofanya na kupelekea
kupata mafanikio makubwa ya mradi huu ambayo yamewafurahisha Wahisani wetu
ambao ni Benki ya Dunia, Shirika la Misaada la Uingereza (DFID) na USAID na
kufikia maamuzi ya kutusaidia tena katika Awamu hii ya tatu. Kwa niaba ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nawashukuru kwa dhati Wahisani hao kwa
misaada yao mikubwa kwa Tanzania na kwa Zanzibar.
MAMBO MUHIMU YALIOJITOKEZA BARAZANI:
13.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa 10 wa Baraza lako
Tukufu, Waheshimiwa Mawaziri wamewasilisha miswada minne (4) ya sheria ambayo
ina umuhimu mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Miswada
iliyowasilishwa na kupitishwa na Baraza lako tukufu ni:
14.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa kwanza uliojadiliwa ni Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria ya Ruzuku kwa Vyama vya Siasa na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo
Nam. 6 ya mwaka 1997. Marekebisho ya Sheria hii yana lengo la kuimarisha
demokrasia nchini mwetu pamoja na kuviongezea uwezo vyama vya siasa kushiriki
katika chaguzi zote zinazoendeshwa nchini.
Mgawanyo wa ruzuku hiyo kwa Vyama vya Siasa utafanywa kwa mujibu wa
utaratibu uliowekwa baada ya Mheshimiwa Rais kuweka saini sheria hiyo.
15.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Pili uliojadiliwa na Baraza lako Tukufu ni Mswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Usafiri wa Baharini Nam. 5 ya mwaka 2006. Mswada huu unakusudia
kuweka mazingira bora ya udhibiti wa masuala ya usafiri wa baharini na
kuhakikisha kuwa yanatekelezwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria hii. Marekebisho
ya Sheria hii yamezingatia maeneo mbali mbali ikiwemo suala la umri wa meli
kutumika kwake tangu ilipoundwa ambayo itaruhusiwa kuingia nchini. Aidha, suala
jengine lililozingatiwa ni kutobadilisha uasili wa meli kutoka kwenye uasili wa
meli ya kubeba mizigo na kuwa meli ya abiria.
Lengo hasa la Mswada huu ni kuwalinda wananchi kutokupoteza maisha yao
kutokana na ajali zisizo na sababu.
16.
Mheshimiwa Spika, pia marekebisho ya sheria hii yana lengo la kuweka uwiano na
mashirikiano mazuri kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha usalama wa usafiri baharini
kutokana na kwamba meli zinasafiri pande zote mbili za Muungano. Haya yote ni
maudhui yaliyozingatiwa kwenye marekebisho ya Sheria ya Usafiri wa Baharini.
17.
Mheshimiwa Spika, marekebisho ya sheria hii pia yanalenga kuweka utaratibu mzuri wa
usafiri wa abiria na mizigo kwa vyombo vya baharini na hivyo kuondoa sababu za
kibinadamu zinazosababisha ajali.
18.
Mheshimiwa
Spika, Mswada mwengine uliowasilishwa na kujadiliwa kwenye Baraza lako
Tukufu ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Shirika la Utangazaji Zanzibar, Kazi,
Majukumu na Utawala wake pamoja na Mambo mengine yanayohusiana na hayo. Mswada
huu unakusudia kufuta Tangazo la Sheria Nam. 111/2011 la kuanzisha Shirika la
Utangazaji Zanzibar pamoja na kazi na majukumu yake. Umuhimu wa kuanzisha upya
Shirika hilo umekuja kutokana na haja ya kuwa na chombo kimoja tu
kitakachosimamiwa na kuendeshwa na uongozi wa aina moja tu ambao ni Mkurugenzi
Mkuu mmoja, Mhariri Mkuu mmoja, Mhandisi Mkuu mmoja na Meneja wa Vipindi.
Utaratibu huu wa sheria hii utaliimarisha Shirika pamoja na kuleta ufanisi
zaidi.
19.
Mheshimiwa Spika, Wajumbe wa Baraza lako wakati wakijadili mswada huu walisisitiza sana
umuhimu wa kuwepo na wataalamu wa fani mbali mbali watakaoweza kuliendesha
Shirika letu la Utangazaji kwenye mazingira yaliopo sasa ya kiushindani kwa
lengo la kuwavutia wananchi.
20.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako pamoja na
wananchi kwamba Serikali imejipanga vyema katika kuliimarisha shirika
kimajengo, vifaa na wataalam, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kuwajengea
uwezo wataalamu hao.
21.
Mhesimiwa Spika, Serikali imo kwenye hatua zake za mwisho za kuondoka kwenye matumizi ya
analogia na kwenda kwenye dijitali. Ni dhahiri kwamba matumizi ya mfumo wa
dijitali yanahitaji utaalamu wa hali ya juu unaoendana na ubunifu ili Shirika
hili liweze kusonga mbele kwa kutoa habari za kisiasa, kiuchumi na kijamii za
ndani na nje ya nchi. Serikali itayazingatia sana maslahi na marupurupu ya
wafanyakazi wa Shirika ili kuwajengea mazingira mazuri ya kuweza kuwajibika
ipasavyo na kuweza kulibadilisha kwa kuimarisha huduma zake ili ziwe nzuri na
za haraka zaidi. Serikali pamoja na
wananchi kwa ujumla wana mategemeo makubwa ya kuona Shirika hili linabadilika
sana na kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea. Huu sasa ni wakati wa
kutoa huduma za kiushindani, kutafuta wateja na kubuni mambo mbali mbali ili
kuweza kukidhi mahitaji ya walengwa.
22.
Mheshimiwa Spika, tunakusudia Shirika hili lijiendeshe kibiashara, hivyo kila atakayetumia
huduma zake, ikiwa ni pamoja na Baraza la Wawakilishi, itawalazimu kuzilipia
huduma hizo.
23.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Nne uliojadiliwa katika Mkutano huu wa 10 wa Baraza lako ni
Mswada wa Sheria ya Kuanzishwa kwa Shirika la Meli Zanzibar Kazi, Uwezo na
Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
24.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Meli hapo awali liliundwa kwa mujibu wa Amri ya Rais
iliyotolewa mwaka 1983 chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Nam. 4 ya mwaka
1978 ambayo imeshafutwa na kwa sasa Mashirika yote ya Umma yanasimamiwa na
Sheria ya Mitaji ya Umma Nam. 4 ya mwaka 2004. Mswada uliopitishwa na Baraza
lako unakusudia kutekeleza Sera ya Usafiri ya Zanzibar pamoja na Mpango Mkuu wa
Usafiri wa mwaka 2008 na kuliwezesha Shirika jipya la Meli kutoa huduma za
usafiri zilizo bora na zinazoendana na matwaka ya viwango vya ushindani wa
Kitaifa na Kimataifa.
25.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina lengo la kuwa na usafiri wa baharini ulio bora zaidi na
endelevu hapa Zanzibar. Sote tunaelewa jinsi nchi yetu ilivyokumbwa na misiba
mikubwa kutokana na kukosa usafiri wa baharini wa uhakika. Nchi yetu ni ya
visiwa ambapo usafiri mkubwa unaotumiwa na wananchi walio wengi ni kwa njia ya
bahari. Serikali yetu imeanza kuchukua jitihada za hali na mali za kuweza
kuagiza meli kubwa, ya uhakika na itakayoweza kuchukua abiria wengi na mizigo
kwa usalama. Kwa mantiki hiyo, Serikali imekusudia kuanzisha Shirika la Meli
litakaloimarisha huduma za meli kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kijamii,
kiuchumi na kibiashara. Aidha, Shirika litasimamia uendeshaji wa meli zetu
kitaalamu na kibiashara ili ipatikane tija na faida ya kuliimarisha shirika hilo.
Serikali itachukua hatua za kuhakikisha kwamba Shirika hili linapatiwa
wataalamu na kuendeshwa kwa ufanisi.
26.
Mheshimiwa Spika, Sheria hizi zote zimetungwa na Baraza lako Tukufu kwa nia ya
kuwatumikia wananchi. Ningependa
kuwasihi watekelezaji wa sheria hizo wazisimamie na kuhakikisha kuwa
zinatekelezwa ipasavyo, bila ya kumuonea haya au aibu mtu yoyote atakayezikiuka
sheria hizi.
27.
Mheshimiwa Spika, mara nyingi Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wamekuwa wakilalamika kuwa
sheria nyingi zimetungwa lakini kumekuwa na udhaifu wa kusimamia utekelezaji
wake. Nakubaliana na malalamiko hayo. Hii ni kwa sababu wasimamizi wa sheria
zinazotungwa hawawajibiki ipasavyo. Kwa
mfano, tuangalie, usimamizi wa Sheria ya Usalama Barabarani. Hausimamiwi vizuri na wahusika. Utaona waendesha baiskeli wakiendesha
baiskeli zao usiku bila taa, magari yanaendeshwa usiku bila namba (Number
plates), hatujui madhumuni yake ni nini, wapanda mapiki piki hawavai kofia za
kinga (helmet), wanaosimamia sheria hizi wapo lakini wanaangalia tu. Nawaomba sasa watekelezaji na wasimamizi wa
sheria hizi watimize wajibu wao. Huu ni
mfano mmoja tu.
28.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha uchumi na kuimarisha shughuli za uwakala,
Serikali inaendelea na juhudi zake za kutafuta Washirika wa Maendeleo na
wawekezaji watakaochangia ujenzi wa bandari mpya ya kibiashara ya Mpiga Duri,
ili Serikali iweze kuongeza mapato yake kutokana na meli kubwa zitakazotumia
bandari hiyo.
29.
Mheshimiwa Spika, Baraza lako Tukufu
liliunda Kamati Teule ya Kuchunguza utendaji wa Shirika la Umeme na Kamati
Teule ya Kuchunguza Utendaji wa Baraza la Manispaa. Nawapongeza kwa dhati
Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati hizi kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kufuatilia
kwa kina masuala mbali mbali kwa mujibu wa hadidu rejea walizopewa na
kuwasilisha ripoti zao katika Baraza hili.
Nawashukuru Wenyeviti wa Kamati hizo kwa umakini wao na kufanya
uchunguzi wa kina kuhusu utendaji katika Taasisi hizo.
30.
Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Baraza lako Tukufu kwamba Serikali imepokea
ripoti hizo za Kamati Teule zilizowasilishwa katika Baraza na itazifanyia kazi
taarifa hizo pamoja na mapendekezo yake kwa umakini mkubwa na kuchukua hatua
kadri itakavyoonekana inafaa. Nirudie
kuwapongeza Viongozi na Wajumbe wote wa Kamati hizi kwa kazi kubwa
waliyoifanya, ambayo Serikali inathamini sana kazi yao hiyo yenye lengo la
kuimarisha utendaji na uwajibikaji Serikalini.
Ningependa kuwahakikishia Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwamba wale wote
waliotajwa kwenye ripoti hiyo watashughulikiwa vipasavyo kwa kuzingatia haki na
utawala bora. Kama baadhi ya Wajumbe
walivyosema, aliyekuwemo hatoki na asiyekuwamo hataingia.
31.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, jumla ya maswali 72
ya msingi na maswali ……… ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wawakilishi na
kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri husika. Nawapongeza sana
Waheshimiwa Wajumbe kwa kuja na maswali mazuri yenye lengo la kujenga zaidi na
kuimarisha uwajibikaji wa watendaji wa Serikali. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa
Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa majibu yao ya kina ambayo hatimaye
yaliwaridhisha Waheshimiwa Wajumbe.
32.
Mheshimiwa
Spika, nachukua
fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako na wananchi wote wa
Zanzibar kwamba Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa
Kitaifa, inayoongozwa na kiongozi makini, Dkt. Ali Mohamed Shein inafanya kazi
kubwa ya kuiletea nchi yetu maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za
jamii. Katika kufanikisha hayo, Serikali
inaendelea na jitihada za kuimarisha sekta za uzalishaji, zikiwemo za kilimo,
mifugo na uvuvi, kuimarisha sekta ya viwanda, utalii na biashara na kuendeleza
sekta ya miundombinu nchini. Vile vile, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya
elimu, afya na kuhakikisha wananchi wote wa mijini na mashamba wanapata maji
safi na salama kwa kuimarisha afya zao na kuwa na nguvu kazi bora
itakayoshiriki katika kukuza uchumi wetu. Lengo kuu la jitihada hizi ni kukuza
uchumi na kupunguza umasikini katika nchi yetu.
33.
Mheshimiwa
Spika, ili
tuweze kufanikiwa katika jitihada
zetu hizi, ni lazima sote tuwajibike katika kutunza mazingira yetu. Hatuna budi
sote kwa pamoja kushiriki kikamilifu katika upandaji wa miti, utuzanji wa
misitu yetu ya asili na kuachana na tabia ya kuchimba mawe na mchanga ovyo bila
ya vibali na kutupa taka ovyo. Aidha, nawataka wafanya biashara ambao bado
wanaendelea na tabia ya kuingiza mifuko ya plastiki nchini waachane na tabia
hiyo mara moja kwani kuendelea kufanya hivyo ni kuhatarisha afya zetu na vizazi
vyetu. Uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu, hivyo kila mwananchi
ana wajibu wa kutunza mazingira kwa manufaa ya nchi yetu.
UNUNUZI WA MELI:
34.
Mheshimiwa
Spika, katika
hotuba yangu wakati wa kufunga Mkutano wa Nane wa Baraza lako Tukufu nilieleza
juhudi inayofanywa na Serikali za kununua meli mpya, kubwa ya abiri
itakayokidhi mahitaji ya usafiri wa baharini katika Visiwa vyetu na katika
maeneo ya mwambao wa nchi jirani.
Napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba Serikali imekwisha chukua
hatua hizo na hivi karibuni Serikali itatiliana saini mkataba na Kampuni ya
Damen ya Uholanzi itakayotengeneza meli hiyo.
Mheshimiwa Spika, meli hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria
wapatao1,200 na mizigo yenye uzito wa tani 200.
Meli hiyo itachukua miezi 18 kutengenezwa baada ya mkataba kuwekwa saini
na pande mbili hizo. Hivyo, wananchi wa
Zanzibar wategemee, kama mambo yote yatakwenda sawa, kupata meli mpya mnamo
robo ya mwisho ya 2014, ingawa inawezekana ikawa zaidi kabla ya hapo.
35.
Mhesimiwa Spika, kwa mara nyengine tena naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe
binafsi, Wajumbe wa Baraza lako, Waandishi wa Habari na wananchi wote kwa
mashirikiano makubwa katika kuliendesha Baraza letu kwa mafanikio. Kadri siku
zinavyoendelea mbele, wananchi wanazidi kujenga matumaini makubwa na Baraza
hili na Serikali yao na hii ndio ishara ya kukua kwa utawala wa demokrasia
nchini.
36.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja ya
kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 3 April, 2013
saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
37.
Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment