Habari za Punde

Mswada ruzuku vyama vya siasa wapita


Na Husna Mohammed
BAADHI ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameshauri kuwa vyama vya siasa vitakavyopata asilimia 10 ya vipewe ruzuku na serikali.

Sambamba na hilo wajumbe hao walipendekeza fedha hizo zifanyiwe ukaguzi   mara baada ya matumizi, jambo ambalo litaepusha ubadhirifu.

Walisema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichoanza jana Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar wakati wakichangia mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya ruzuku kwa vyama vya siasa nambari 6 ya 1997.

Walisema iwapo kama ruzuku hiyo itagawiwa kwa vyama vilivyopata asilimia kumi ni wazi kuwa itaweza kuepuka kuanzishwa vyama vyengine ambavyo vitakuwa na lengo la kupata ruzuku bila ya kuzingatia ushindani wa kisiasa.


Akichangia mswada huo, Mwakilishi wa Magomeni, Salmin Awadh alisema kigezo cha mgao huo kwa kiasi kikubwa kutaepusha utitiri wa vyama ambavyo vitategemea kupata ruzuku.

“Watu wataona huo ndio ulaji kama ruzuku itatolewa bila masharti na hivyo hakutakuwa na ushindani wa kivyama na badala yake vyama vitafuata ruzuku tu, pia iwapo kama vyama vilivyopata asilimia kumi ya kura vitapata ruzuku basi vyama vyengine vilivyopo vitaweza kutumia ushindani wa kidemokrasia ili kuona vinapata nafasi ya kupata kura,” alisema.

Nae Mwakilishi wa jimbo la Chonga, Abdalla Juma, alipendekeza ruzuku hiyo itolewe kwa vyama vitakavyopata asilimia 20 ya kura.

“Asilimia moja ni kubwa kwa kuwa fedha hizi ni za walipa kodi hivyo ni lazima kudhibiti matumizi makubwa ya walipa kodi wetu,” alisema.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma, aliliafiki pendekezo la kupewa ruzuku kwa vyama vitakavyoshinda kwa asilimia kumi ya kura.

Hata hivyo, alipendekeza kufanyiwa ukaguzi wa kina kwa matumizi ya fedha kwa vyama vitakavyopata ruzuku hiyo.

Mwakilishi wa Kitope, Makame Mbarouk Mshimba, aliiomba serikali kuangalia kwa makini matumizi ya fedha hizo hasa ikizingatiwa kuwa ni za walipa kodi walio wanyonge.

“Ni bora tukawaangalia hawa watumishi wetu wa umma, mishahara yao ni midogo na maisha yamepanda hivyo ni vyema hizo fedha tukazielekeza kwao,” alisema.

Pia alisema serikali ni vyema ikaangalia kuongeza vyanzo vya mapato kabla ya kuziidhinisha na kuruhusu fedha hizo kutumika kwa vyama vya siasa.

Mapema akiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya ruzuku kwa vyama vya siasa namba 6 ya mwaka 1997, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema madhumuni serikali ni kutimiza wajibu wake wa msingi wa kuimarisha demokrasia na utawala bora nchini.

Alisema kwa kuwa vyama vya siasa ni nguzo kuu ya demokrasia na  uwakilishi hivyo ni lazima vipate ruzuku kama zinavyotoa nchi nyengine duniani.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha sheria hiyo ni lazima asilimia 50 ya ruzuku kIpewa chama kilichopata kiti cha urais, asilimia 30 kugaiwa uwiano wa viti vya majimbo ya wawakilishi na asilimia 20 uwiano wa viti vya wadi.

“Kwa kuliona hilo serikali imechukua hatua ya kushauriana na wadau wa sheria na wamechangia kwa kina katika mapendekezo yanayowasilishwa na serikali,” alisema.

Mapema akiwasilisha maoni ya kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya  kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa kuhusu mswada wa sheria hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Mwanajuma Faki Mdachi, alishauri kuwepo asilimia  maalumu kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi za kitaifa hata kama kura za wananchi hazikutosheleza kuviwezesha vyama hivyo kushinda.

Aidha alisema vyama vya siasa vipewe ruzuku kwa ajili ya kuimarisha demokrasia ya ushindani wa kisiasa pamoja na uhai wa vyama hivyo.

Baada ya mjadala na michango Mswada huo umepitishwa rasmi jana jioni.

1 comment:

  1. masikini laiti mngalijua mnafanya nini nyie mnaojiita wawakilishi msingepitisha muswada huu , sishangai kwani wengi wenu nyie wawakilishi ni pumba hamna shule , mmekwisha sasa matokea yake mtayajua baada ya muda mfupi tu , na hilo ni pigo kubwa wa wale wanaoataka znz kuwa huru

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.