Na Husna Mohammed
BAADHI ya wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wameshauri kuwa vyama vya siasa vitakavyopata asilimia 10 ya vipewe
ruzuku na serikali.
Sambamba na hilo wajumbe hao
walipendekeza fedha hizo zifanyiwe ukaguzi
mara baada ya matumizi, jambo ambalo litaepusha ubadhirifu.
Walisema hayo katika kikao cha
Baraza la Wawakilishi kilichoanza jana Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar wakati
wakichangia mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya ruzuku kwa vyama vya
siasa nambari 6 ya 1997.
Walisema iwapo kama
ruzuku hiyo itagawiwa kwa vyama vilivyopata asilimia kumi ni wazi kuwa itaweza
kuepuka kuanzishwa vyama vyengine ambavyo vitakuwa na lengo la kupata ruzuku
bila ya kuzingatia ushindani wa kisiasa.
Akichangia mswada huo, Mwakilishi
wa Magomeni, Salmin Awadh alisema kigezo cha mgao huo kwa kiasi kikubwa
kutaepusha utitiri wa vyama ambavyo vitategemea kupata ruzuku.
“Watu wataona huo ndio ulaji kama
ruzuku itatolewa bila masharti na hivyo hakutakuwa na ushindani wa kivyama na
badala yake vyama vitafuata ruzuku tu, pia iwapo kama vyama vilivyopata
asilimia kumi ya kura vitapata ruzuku basi vyama vyengine vilivyopo vitaweza
kutumia ushindani wa kidemokrasia ili kuona vinapata nafasi ya kupata kura,”
alisema.
Nae Mwakilishi wa jimbo la Chonga,
Abdalla Juma, alipendekeza ruzuku hiyo itolewe kwa vyama vitakavyopata asilimia
20 ya kura.
“Asilimia moja ni kubwa kwa kuwa
fedha hizi ni za walipa kodi hivyo ni lazima kudhibiti matumizi makubwa ya
walipa kodi wetu,” alisema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wawi,
Saleh Nassor Juma, aliliafiki pendekezo la kupewa ruzuku kwa vyama
vitakavyoshinda kwa asilimia kumi ya kura.
Hata hivyo, alipendekeza kufanyiwa
ukaguzi wa kina kwa matumizi ya fedha kwa vyama vitakavyopata ruzuku hiyo.
Mwakilishi wa Kitope, Makame
Mbarouk Mshimba, aliiomba serikali kuangalia kwa makini matumizi ya fedha hizo
hasa ikizingatiwa kuwa ni za walipa kodi walio wanyonge.
“Ni bora tukawaangalia hawa
watumishi wetu wa umma, mishahara yao ni midogo na maisha yamepanda hivyo ni
vyema hizo fedha tukazielekeza kwao,” alisema.
Pia alisema serikali ni vyema
ikaangalia kuongeza vyanzo vya mapato kabla ya kuziidhinisha na kuruhusu fedha
hizo kutumika kwa vyama vya siasa.
Mapema akiwasilisha mapendekezo ya
marekebisho ya sheria ya ruzuku kwa vyama vya siasa namba 6 ya mwaka 1997,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed,
alisema madhumuni serikali ni kutimiza wajibu wake wa msingi wa kuimarisha
demokrasia na utawala bora nchini.
Alisema kwa kuwa vyama vya siasa ni
nguzo kuu ya demokrasia na uwakilishi
hivyo ni lazima vipate ruzuku kama zinavyotoa
nchi nyengine duniani.
Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 5
cha sheria hiyo ni lazima asilimia 50 ya ruzuku kIpewa chama kilichopata kiti
cha urais, asilimia 30 kugaiwa uwiano wa viti vya majimbo ya wawakilishi na
asilimia 20 uwiano wa viti vya wadi.
“Kwa kuliona hilo serikali
imechukua hatua ya kushauriana na wadau wa sheria na wamechangia kwa kina
katika mapendekezo yanayowasilishwa na serikali,” alisema.
Mapema akiwasilisha maoni ya kamati
ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa
kuhusu mswada wa sheria hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Mwanajuma Faki Mdachi,
alishauri kuwepo asilimia maalumu kwa
vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi za kitaifa hata kama kura za wananchi
hazikutosheleza kuviwezesha vyama hivyo kushinda.
Aidha alisema vyama vya siasa vipewe
ruzuku kwa ajili ya kuimarisha demokrasia ya ushindani wa kisiasa pamoja na
uhai wa vyama hivyo.
Baada ya mjadala na michango Mswada
huo umepitishwa rasmi jana jioni.
masikini laiti mngalijua mnafanya nini nyie mnaojiita wawakilishi msingepitisha muswada huu , sishangai kwani wengi wenu nyie wawakilishi ni pumba hamna shule , mmekwisha sasa matokea yake mtayajua baada ya muda mfupi tu , na hilo ni pigo kubwa wa wale wanaoataka znz kuwa huru
ReplyDelete