Joseph Ngilisho, Arusha
SERIKALI imeanza kutekeleza
mpango wa kuwajengea uwezo wakaguzi wa
ndani wa umma ili waweze kushiriki kikamilifu katika mabadiliko baada ya
kuridhia mwongozo wa viwango vya kimataifa uliotolewa mwaka 2011.
Kauli hiyo imetolewa jana
na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa serikali , Mohamed Mtonga wakati akifungua
mafunzo ya siku tatu kwa wakaguzi wa ndani wa serikali kanda ya kaskazini.
Alisema mkutano huo unalenga kuwajengea uwezo
wakaguzi wa ndani jinsi ya kuandaa miongozo inayoendana na maadili ya shughuli
zao huku ikizingatia viwango vya ukaguzi wa kimataifa.
Mtonga alisema katika kuridhia
mpango huo wa ukaguzi wa ndani katika
sekta ya umma ni lazima uzingatie
viwango vya kimataifa ili kuongeza uwajibikaji katika sekta ya umma.
“Ili kuhakikisha ukaguzi huo
unaendana na viwango vya kimataifa lazima kutayarishwe mfumo maalumu wa uhakiki
wa ubora wa ukaguzi wa ndani ambapo
swala la maadili na uwajibikaji wa wakaguzi wa ndani litapewa uzito wa kutosha
katika mfumo huo mpya nah ii ndio njia pekee itakayowezesha kuboresha shughuli
zao,” alisema Mtonga.
Alisema wanataka wakaguzi wa ndani
kufanya shughuli zao kwa uhuru zaidi
bila kuingiliwa na mtu yeyote na hatimaye kuweza kuleta taarifa sahihi
kuhusiana na ukaguzi wao.
Alifafanua zaidi kuwa, baada ya
mafunzo hayo wakaguzi wa ndani wataweza kutoa huduma kwa viwango vinavyotakiwa
huku wakifanya kazi zao kwa kufuata maadili na miongozo waliyopewa na hiyo
itawezesha kuboresha utendaji kazi wao kwa ujumla.
Mafunzo hayo ya siku tatu ya
wakaguzi wa ndani wa umma kanda ya kaskazini ni ya pili kufanyika ambapo
lengo la serikali ni kuendesha mafunzo kama
hayo katika kanda zote nchini.
No comments:
Post a Comment