JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME
YA MABADILIKO YA KATIBA
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ufafanuzi
kuhusu Utaratibu wa Kuwasilisha Maoni ya Makundi kuhusu Katiba
Alhamisi, Januari 17,
2013
Tume ya Mabadiliko ya
Katiba inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoandikwa na vyombo
mbalimbali vya habari yakiwemo baadhi ya magazeti Alhamisi, Januari 17, 2013 ambazo
zinazoashiria kuwa Tume inakataa kupokea baadhi ya maoni yanayowasilishwa kwake
na makundi mbalimbali.
Taarifa hizo za vyombo vya habari zimetokana na
kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Dkt.
Ramadhan Mlinga aliyoitoa mara baada ya taasisi yake kuwasilisha kwa Tume maoni
kuhusu Katiba Mpya siku ya Jumatano, tarehe 16 Januari, 2013 katika Ukumbi wa
Karimjee jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa
hizo, mara baada ya PPRA kuwasilisha maoni kwa Tume, Wajumbe wa Tume walisita
kupokea maoni ya taasisi hiyo na badala yake kuagiza PPRA kuandaa maoni tena na
kuyawasilisha katika Tume ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe 16
Januari, 2013.
Kufuatia taarifa hizo,
Tume inapenda kuwataarifu wananchi, makundi, taasisi na wadau wengine wote kuwa
Tume haijakataa na haina mamlaka ya kisheria ya kukataa kupokea maoni ya mtu, jumuiya,
taasisi au kundi lolote.
Katika mikutano
inayoendelea, kabla ya kuhitimisha mkutano husika, Tume huomba chama cha siasa,
jumuiya, taasisi au mtu aliyewasilisha maoni kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali
zilizojitokeza katika kikao. Ufafanuzi huu hutolewa kwa hiari palepale katika mkutano
au kwa maandishi baada ya siku kadhaa ambazo Tume hukubaliana na mtu au kikundi
kilichowasilisha maoni.
Mikutano
inayoendelea kati ya Tume na Makundi mbalimbali
inafuatia kukamilika kwa mikutano ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi tarehe
19 Disemba mwaka jana (2012).
Kwa msingi huu, katika
mkutano kati ya Tume na PPRA uliofanyika juzi tarehe 15 Januari, 2013, Tume
iliiomba PPRA kuangalia uwezekano wa kutoa ufafanuzi wa masuala ya ziada ambayo
Tume ilitaka kupata maoni ya kitaalamu kutoka katika taasisi hiyo. Ombi kama
hili pia limetolewa kwa makundi mengine ambayo yameshakutana na Tume kutoa
maoni kuhusu Katiba Mpya.
Mwisho.
Imetolewa
na:
Bw.
Assa Rashid
Katibu,
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba,
S.L.P.
1681,
DAR
ES SALAAM
0757-500800
No comments:
Post a Comment