Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk Amani Abeid Karume akikagua baadhi ya madarasa ya skuli ya Secondary ya Donge Muanda ilioko huko Kaskazini Unguja. |
Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk Amani Abeid Karume akikunjuwa Kitambaa kuashiria Ufunguzi wa Skuli ya Secondary huko Donge Muanda Kaskazini Unguja. |
Na Ali Issa Maelezo Zanzíbar.
Rais mstaafu awamu ya sita wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzíbar Dkt. Amani Abeid Karume amewataka Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Muwanda kujikita zaidi katika masomo ya Sayansi ili kupata Wataalamu wa masomo hayo watakaoendana na maendeleo ya kisasa.
Amesema Wanafunzi hao wanapaswa kuyapa kipaumbele masomo hayo kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzíbar imegharamika kuleta Walimu wa masomo ya Sayansi kutoka Nchini Nageria na Skuli hiyo kubahatika kupata Walimu hao.
Dkt. Karume ameyasema hayo huko Donge Muwanda wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Donge ikiwa ni shamra shamra za sherehe ya kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzíbar.
Amesema fursa hiyo waitumie kwa kushirikiana na wataalamu walipo ili waweze kufaulu mitihani yao na hatimaye kujiunga Vyuo vikuu kupitia masomo ya Sayansi.
“Tunahitaji Marubani,Mainjinia,Madaktari nk, na vyuo vya kusomea vipo,hivyo jifuzeni masomo haya ambayo ndiyo kipaumbele kwa sasa” Alisisitiza Dkt. Karume.
Aidha Dkt. Karume alisema kuwa Wanamapinduzi huangalia mbele wanapoekeza mambo yao ya kimaendeleo ambapo kwa sasa Masomo ya Sayansi ndio ambayo yanaweza kupelekea maendeleo kwa Wananchi wa Donge na Zanzíbar kwa ujumla.
Dkt. Karume aliwataka wazazi na wanakamati wa Skuli hiyo kuwahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na waache michezo kwani mtoto akiwa mdogo huwa hafahamu umuhimu wa elimu.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Donge Ali Juma Shamhuna alisema Skuli hiyo itakuwa ya Wilaya kwa masomo ya Sayansi ambapo anatarajia kupata walimu wengine wa Sayansi baada ya kuwaajiri walimu wapya waliohitimu Chuo kikuu cha Tungu hivi karibuni.
Aidha Waziri huyo aliwahakikishia Wananchi wa Donge kujenga uzio wa Skuli hiyo,kujenga kiwanja cha michezo, Dahalia, Msikiti na kuimalizia barabara kutoka Donge hadi Muwanda.
Mradi wa ujenzi wa skuli hiyo yenye madarasa 12, Maabara tatu,Maktaba moja na Nyumba tatu za Walimu umefanikiwa kutokana na Mkopo wa Banki ya Dunia,ambapo pia utajumuisha ujenzi wa Skuli nyingine 27 katika maeneo Mbali Mbali ya Unguja na Pemba.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment