Habari za Punde

Serikali itahakikisha kila mtoto aliyefikia umri wa kusoma anapata nafasi ya kusoma

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa lengo la Serikali anayoiongoza ni kuhakikisha kuwa kila mtoto aliyefikia umri wa kusoma anapata nafasi ya kusoma kwani kabla ya Mapinduzi hapakuwa na fursa hiyo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja wakati akiifungua skuli mpya ya Sekondari ya Umoja ya Uzini ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za sherehe ya kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa malengo ya Mapinduzi yalikuwa ni kuimarisha sekta za maendeleo kwa kuhakikisha wananchi wote wanapata fusa sawa tena bila ya ubaguzi pamoja na kuirejesha heshimwa ya mwananchi wa Zanzibar.
Alisema kuwa kabla ya Mapinduzi elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi na kwa matabaka maalum hali ambayo iliwanyima fursa wananchi waliowengi ambao walikuwa ni wanyonge na kusisitiza kuwa hata hizo skuli zenyewe kwa wakati huo hazikuwepo za kutosha.
Kutokana na hali hiyo mara tu baada ya Mapinduzi Rais wa Awamu ya Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alitangaza elimu bila Malipo ikiwa ni pamoja na kuzi
Alieleza kuwa jambo kubwa hivi sasa linalopewa kipaumbele na serikali ni kuifanya elimu iwe bora zaidi hapa Zanzibar kwani tayari juhudi za kujenga majengo ya skuli Unguja na Pemba zimekuwa zikichukuliwa siku hadi siku licha ya changamoto ya kuwepo kwa wanafunzi wengi katika madarasa hasa kwa upande wa skuli za msingi.
Dk. Shein aliwataka wazee na waalimu kuhakikisha wanatoa msaada mkubwa kwa vijana ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao kwani wao wana nafasi kubwa katika maendeleo ya vijana hao.
Alisema kuwa mkazo mkubwa hivi sasa unapelejkwa katika elimu ya sayansi bila ya kupunguza kasi katika masomo mengine yaliobaki.
Dk. Shein alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha fedha zilizojenga skuli hizo 21 hapa Zanzibar zinapatikana na inakabidhiwa Zanzibar katika kutekeleza mradi huo wa uimarishaji wa elimu ya lazima (ZABEIP).
Pamoja na hayo, Shein alieleza matumaini yake kwa Benki ya dunia kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza mradi huo kwa awamu ya pili ikiwa ni pamoja na kujenga daghalia na nyumba za walimu.
Dk. Shein pia, alisisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar kwani ndio nguzo ya maendeleo na kueleza kuwa pahala penye mfarakano kamwe maendeleo hayapatikani.
Alieleza kuwa Skuli mpya ya Umoja ya Uzini ni miongoni mwa skuli mpya 21 alizoahidi wakati akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 na kusisitiza kuwa uzinduzi kama huo unafanyika kwa skuli nyengine zikiwemo Dole, Chaani, Matemwe na Muwanda kwa Unguja na Ngwachani, Wawi na Shamiani kwa upande wa Pemba.
Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara, Benki ya Dunia pamoja na kampuni ya Ujenzi ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd chini ya mtaalamu wake Bi Mariam Ma kutoka China kwa ujenzi mzuri wa skuli hiyo pamoja na ile ya Dole.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Ali Juma Shamuhuna alisema kuwa Benki ya dunia imeonesha azma ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kutekeleza awamu ya pili ya ujenzi wa skuli hizo ambapo itakuwa ni daghalia na nyumba za walimu.
Pia, Shamuhuna alisema kuwa Zanzibar imo katika kutekeleza Malengo ya Milenia ya kuhakikisha watoto wote waliofika umri wa kusoma wanapata fursa hiyo ifikapo mwaka 2015, ambapo kwa upande wa Zanzibar hatua hiyo imeshafikiwa.
Alieleza kuwa mbali ya kuwaleta waalimu kutoka nchi za nje kama vile, Nigeria ambao wapo hivi sasa na nchi nyengine ambazo zimeahidi zikiwemo Misri, Ghana, Pakistan, India, Marekani na Uingereza, Serikali imo katika mikakati ya kuwasomesha waalimu wake wenyewe ili waje kusomesha masomo ya Sayansi na mengineyo.
Mapema Naibu Katibu wa Wizara hiyo, Maalim Abdala Mzee alisema kuwa gharama ya skuli hiyo ni Bilioni moja mbali ya vifaa na thamani zilizomo katika skuli hiyo.
Alieleza kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 62.7 zinatarajiwa kutumika katika mradi huo ambapo utakuwa na skuli 19 za Sekondari,pamoja na chuo cha waalimu huko Pemba na skuli 6 za sekondari zinazofanyiwa matengenezo pamoja na vifaa, vitabu, thamani na mafunzo ya waalimu..

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.