Habari za Punde

Ukahaba wamtia kiwewe RC

Na Kija Elias, Moshi 

BIASHARA ya ukahaba iliyoshamiri katika maeneo mbali mbali ya mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro, imemchafua Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, ambaye ametangaza mpango maalum wa kudhibiti vitendo hivyo.

 Gama alisema kushamiri kwa biashara hiyo haramu, katika maeneo miji katika mkoa huo imekuwa sababu kubwa ya kurudisha nyuma harakati za mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi. 

Aliyasema hayo juzi kwenye mkutano na waandishi wa habari, huku akizungumzia mafanikio ya maendeleo ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2005/2012 mkoani Kilimanjaro. 


Alisema biashara ya ngono imeshika kasi katika manispaa ya Moshi, licha ya kudhibitiwa kwa kipindi cha nyuma, wahusika wameanza kurejea kwa kasi katika maeneo ya starehe wanakofanyia biashara hiyo. 

 Mkuu huyo alitoa agizo kwa jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro, kufanya doria kuwadhibiti wale wanaojihusisha na biashara hiyo, pamoja na halmashauri zote za wilaya kuhakikisha zinajipanga kushirikiana na jeshi hilo kukomesha biashara hiyo ambayo imeuchafua mkoa huo. 

 Kwa mujibu wa taarifa ya mkoa, mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya ukimwi , kabla ya hatua mbali mbali kuchukuliwa kukabiliana na kasi hiyo. Gama alisema, mkoa umefanikiwa kuvuka lengo la kampeni ya kitaifa ya upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa asilimia 146,na kuongezeka vituo vya tiba ya kupunguza makali ya VVU, kutoka 96 mwaka 2004 hadi 32,008 mwaka 2011. 

 Aliongeza kuwa tathmini iliyofanywa ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi wameongezeka kutoka 53 hadi kufikia wagonjwa 18,208 kwa kipindi hicho. 

“Tunachojivunia kwa sasa kama mkoa ni kuongeza vituo vya kutoa ushauri nasaha na upimaji kwa hiari kutoka vituo sita mwaka 1995 hadi vituo 233 mwaka 2011,” alisema Gama. 

 Katika hatua nyingine Gama alisema  kupanuka kwa huduma hizo kumesaidia mkakati wa kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka asilimia 7.3 mpaka asilimia 1.9, kutokana na utafiti wa viashria vya VVU na ukimwi wa mwaka 2007/2008. 

 Mkuu wa mkoa alisema mkakati wa taifa wa kudhiditi ukimwi wa mwaka 2003/2007 na mwaka 2008/2012 mafanikio hayo yalitokana na juhudi mbali mbali zilizofanywa serikali kwa kushirikiano na wadau.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.