Habari za Punde

ZAT walalamikiwa kunyima likizo wafanyakazi


Na Hafsa Golo
WAFANYAKAZI wa kampuni ya utoaji huduma katika uwanja wa ndege wa Zanzibar (ZAT) wamelalamika vitendo vya kunyimwa likizo, kwa kile kilichodaiwa na wafanyakazi hao kuwa kampuni hiyo inajali zaidi maslahi yake.

Mmoja ya wafanyakazi hao, ambae anafanyakazi kama mwangalizi ‘supervisor’ (jina tunalihifadhi), alisema hajapewa likizo kwa vipindi vitano sasa na kila anapoomba anaambiwa asubiri.

Alisema licha ya kuambiwa asubiri kutoka na sababu mbali mbali ikiwemo kuwepo wageni wengi, lakini hapewi mafao yake ya kuzuiliwa likizo yake kama sheria inavyoagiza.

Alisema kwa mara ya mwisho alipewa likizo mwaka 2007.

“Mimi nataka kwenda likizo, sina haja ya kulipwa mafao ya kukatishwa likizo yangu, nataka kupumzika,” alisema.


Alisema kitendo hicho ni cha uonevu na unyanyasaji lakini pia ni ukiukaji wa haki za mfanyakazi kisheria.

Lakini Msaidizi Meneja wa kampuni hiyo, Hassan Mussa alikanusha madai hayo ambapo alisema kutokana na uelewa alionao katika kampuni hiyo hakuna mfanyakazi anaeomba likizo akanyimwa kwa sababu ni haki ya  mfanyakazi kisheria hivyo hakuna sababu ya kumnyima.

Alisema hakuna hata mfanyakazi ambae anadai likizo tano bila kupewa kwa sababu kampuni inahofia kuwa bila ya mfanyakazi kupewa likizo anaweza kufanya kazi chini ya kiwango na kusababisha athari kwa kampuni na abiria.

Hata hivyo, alikiri kwamba kuna baadhi ya wakati  huwataka wafanyakazi wake kuaihirisha likizo yao kutoka kwa kuwepo wageni wengi  lakini kipindi hicho kinapomaliza mfanyakazi huyo hupewa likizo yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.