Habari za Punde

Watoto wachanga 724 walifariki Mnazimmoja, Mwembeladu



Na Asya Hassan
WAJAWAZITO 16,277 walijifungua katika hospitali za Mnazimmoja na Mwembeladu mwaka uliopita ambapo kati yao zaidi ya 20 walifariki dunia.
Watoto 16,187 walizaliwa katika hospitali hizo mbili ambapo kati yao 724 walifariki dunia kutokana na sababu mbalimbali.
Aidha wajawazito waliojifungua wakiwa chini ya umri wa miaka 20 walikuwa 2,045, ambapo hospitali ya Mnazimmoja walijifungua 1,871 na Mwembeladu 174.
Waliojifungua wakiwa na umri wa kuanzia miaka 35 walikuwa 2,232, ambapo Mnazimmoja walikuwa 1,738 na Mwembeladu walikuwa 494.
Wajawazito waliojifungua kwa upasuaji walikuwa 1,679, ambapo Mnazimmoja walikuwa 1,667  na Mwembeladu walikuwa 12 ambapo walifanya kwa majaribio.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana na gazeti hili, pia zinaonesha wajawazito 75 walijifungulia nyumbani na baadae kukimbizwa katika hospitali hizo mbili baada ya kupata matatizo.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wauguzi wa hospitali ya Mnazimmoja ambao hawakutaka majina yao yachapishwe, walisema  idadi ya vifo vya mama wajawazito imepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Hata hivyo, walisema takwimu zinaonesha vifo kwa ujumla vimepungua kutoka na huduma bora pamoja na hamasa waliyonayo wajawazito wa kuvitumia vituo vya afya na hospitali kujifungua.
Waunguzi hao walisema, hata hivyo tokea kuanza huduma bure kwa wajawazito, wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya kuzalisha pamoja na dawa ambazo mjamzito anapaswa kupatiwa baada ya kujifungua.
Kwa mfano walisema wakati mwengine wanakabiliwa na upungufu wa bomba za sindano, ingawa dawa zinapatikana.
Walisema upungufu mwengine unaowakabili ni nyuzi za kushonea na sindano zake ambazo ziliopo sasa ni ndogo, mipira ya kutandika kitandani, mirija ya dripu na glovu.
Waliiomba wizara ya afya kuongeza vifaa katika wodi za wazazi ili kuzifanya huduma za uzazi kutolewa kwa ufanisi zaidi.
Katibu wa hospitali ya Mnazimmoja, Omar Abdalla akizngumza kwa simu alikiri kuwepo kwa upungufu wa vifaa hivyo, hata hivyo alisema juhudi zinachukuliwa kuhakikisha upungufu huo unadhibitiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.