Habari za Punde

Wajumbe wa kamati ya pamoja ya SMT na SMZ wakutana

Na Othman Khamsi Ame, OMPR
Wajumbe wa Kamati ya pamoja kati Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekutana katika utaratibu wao wa kawaida wa kujadili masuala yanayohusu Muungano.
Kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Moh’d Gharib Bilal na kushirikisha Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi,Mawaziri wa SMT,SMZ na baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali zote mbili kilifanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Wajumbe wa Kikao hicho walipitia na kuridhia kumbukumbu za Kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Tarehe 28 Januari mwaka 2012 Mjini Dar es salaam pamoja na kupokea Taarifa ya utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Aidha wajumbe hao walipitia na kuridhia mapendekezo kuhusu utaratibu wa muda wa mgao wa ajira kwa Taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kupitia makubaliano ya hoja zilizopatiwa ufumbuzi.
Wakichangia Hoja mbali mbali zilizowasilishwa kwenye Mkutano huo baadhi ya Wajumbe wa Kikao hicho wameelezea kuridhika kwao na hatua zinazochukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na ile ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar chini ya usimamizi wa Wanasheria Wakuu wa Pande zote mbili katika kulishughulikia suala la mafuta na gesi kuondolewa katika mambo ya Muungano.
Walisema hatua ya kuridhiwa na kukubaliwa na Maraisi wa Serikali zote mbili Nchini limewawezesha na kuwapa nguvu wataalamu wa sheria wa pande zote mbili kuangalia namna ya kuandaa utaratibu utakachokidhi mahitaji ya kisheria ya kila upande kuhusu suala hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alisema mwenendo mzima wa utekelezaji wa masuala yanayoleta kero ndani ya Muungano unakwenda vyema kufuatia mfumo wa vikao vinavyohusisha watendaji wa pande zote mbili.
Waziri Samia alisema hata hivyo yapo baadhi ya masuala ambayo huchukuwa muda mrefu kuyapatia ufumbuzi kutokana na mfumo wa sheria unaohitaji mabadiliko ili kwenda sambamba na makubaliano yaliyoridhiwa.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda akitoa shukrani zake aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maadhimisho mazuri ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za Mwaka huu zilizokuwa za mfano wa aina yake.
Mh. Pinda alisema jamii ingependa kuona sherehe za Mapinduzi za Mwakani kutimia nusu karne zikawa za mafanikio makubwa zaidi na Serikali ya Muungano wa Tanzania inaandaa fikra ya namna ya kuongeza nguvu za ushiriki na mchango wake katika kufanikisha sherehe hizo.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema umahiri wa Mawaziri wa Pande zote mbili katika kikao chao cha sekreterieti umewezesha kamati ya pamoja ya SMT na SMZ kufanikiwa kwa hali ya juu.
Balozi Seif alifahamisha kwamba wajumbe wa kikao hicho wameweza kupokea na kuridhia masuala mbali mbali waliyoyaagiza katika kikao cha mwaka jana ambayo yalikuwa yakileta kero katika masuala ya Muungano.
Akikifunga kIkao Hicho Mwenyekiti wa Kamati ya pamoja na Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Mohd Gharib Bilal alishauri Viongozi wa Wizara za Serikali zote mbili kuendelea kushirikiana ili kuleta ufanisi zaidi.
Dr. Bilal alisema ushirikiano huo utakaoshirikisha pia watendaji na wataalamu wa sekta husika ndani ya taasisi zao utasaidia kupunguza na hatimae kuondosha kabisa kero zinazosababisha hitilafu ndani ya mfumo wa Muungano.
Masuala yaliyowasilisha katika kikao hicho cha Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ na kupokewa na kuridhiwa na wajumbe hao ni pamoja na uwezo wa SMZ kukopa nje ya Nchi, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, kodi ya mapato-pay as you earn { PAYE} pamoja na suala la Mafuta la kutaka kutolewa katika mambo ya Muungano.
Kikao kijacho cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kinatarajiwa kufanyika mara baada ya Sherehe za mwaka huu za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kufanyika pahali zitakapofanyika Sherehe hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.