Habari za Punde

Wanafunzi chuo kikuu Chukwani watumia maji chumvi


Na Juma Khamis

WANAFUNZI wa chuo kikuu cha elimu kishiriki Chukwani, bado wanaendelea kutumia maji ambayo yamechanganyika na chumvi.

Tatizo hilo ambalo limesababishwa na mabadiliko ya tabianchi, linawaathiri kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa chuo.

Wakizungumza katika mahafali ya 12 ya chuo hicho jana, wanafunzi hao waliziomba mamlaka zinazohusika kuingilia kati ili kunusuru hali hiyo ambayo imeanza kuwaathiri.

Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dk. Hikmany Rashid, alisema tayari uongozi wa chuo umewasiliana na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kulishughulikia tatizo hilo.


Changamoto nyengine ambayo wanafunzi hao walizibainisha ni upungufu wa vitabu katika maktaba za chuo na tatizo la ajira hasa kwa wahitimu wa fani ya kiarabu na dini ya kiislamu.

Mapema akihutubia katika mahafali hayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna alikisifu chuo hicho kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya elimu nchini kwa kuendeleza kuzalisha walimu wenye ubora.

Alivihimiza vyuo vikuu kuendelea kufanya tafiti na kuahidi kwamba serikali zote mbili zitaendelea kuzifanyia kazi tafiti zilizofanywa na watalaamu wa vyuo vikuu.

Aidha aliwaasa wahitimu kuitumia elimu waliyopata kwa ajili ya kuitumikia jamii, akisema elimu ni silaha muhimu katika kuleta mageuzi duniani.

Wanafunzi 242 walitunukiwa shahada katika masomo ya sayansi na sanaa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.