Na Rose Chapewa, Morogoro
KUNDI la watu 100
limevamia kituo cha polisi
cha Wilaya ya Gairo mkoani
Morogoro, likishinikiza wenzao watano waachiwe huru baada ya kukamatwa kwa
tuhuma za kuchoma nyumba za mwanakijiji mwenzao kwa madai kuwa alikuwa akizuia
mvua isinyeshe.
Akizungumza na waandishi wa
habari Kamanda wa polisi mkoani hapa,
Faustine Shilogile alisema tukio hilo lilitokea jana saa tatu asubuhi katika kituo kidogo cha
Gairo ambapo kati ya kundi hilo watu 14 walikamatwa wakiwemo wanawake wawili.
Alimtaja Mwanakijiji
aliyechomewa nyumba kuwa ni Andrew Nyangwa (63) mkazi wa kijiji cha Mjawanga
wilayani humo, ambapo alichomewa nyumba tatu zote zikiwa na thamani ya shilingi
milioni 2.8, wakimtuhumu kuzuia mvua isinyeshe yeye pamoja na wenzake ambao majina
yao hayajafahamika.
Aliwataja waliokamatwa kwa
tuhuma za kuchoma nyumba hiyo kuwa
Wilson Msumi (60), Jeremiah Msonga (45), William Semwenda (70), Saimon Mahuma
(80) na Mwigen Malindo (60)) nakwamba
watu hao walichoma nyumba hiyo Februali 17 mwaka huu.
Kamanda Shilogile aliwataja
waliokamatwa kwa kuvamia kituo hicho kuwa ni Saimon Honya (37), Samson acahiuyo (44), Fanuel Muya
(40), Piason Msela (40) John Muya (50) na Charles Chiduo (32), Maneno MSEGU
(29), Petro Chosongel (36), Charles Mangwa (40), Jonas Daomon (20), John
Mziwanda (37),Helena Mwidango (13) Janeth Chiang’ole (57) na Jonas Mlahagwa
(30), na kwamba watafikishwa mahakamani
wakati wowowte baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha Kamanda huyo aliwataka
wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kwenda
kutoa taarifa polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa watuhumiwa.
Hata hivyo alisema jeshi
hilo pia halitawavumilia wananachi ama kundi linalohamasisha uchomaji matairi
moto barabarani pamoja na kuweka magogo, maandamano yasiyo ya msingi wala
vibali, na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wanaojihusisha
na vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment