ADDIS ABABA, Ethiopia
MKATABA wa kumaliza vita Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo umetiwa saini jana mjini Addis Ababa na viongozi wa nchi
za maziwa makuu.
Mkataba huo uliafikiwa kwa
upatanishi wa Umoja wa Mataifa.
Mkataba huo sasa unatoa
nafasi ya kutumwa wanajeshi wa kusimamia amani katika eneo hilo.
Viongozi hao walishindwa
kutia saini mkataba huo mwezi uliopita kutokana na mzozo juu ya nani anapaswa
kukiongoza kikosi cha kulinda amani kitakachowekwa Mashariki mwa DRC.
Kutiwa saini kwa mkataba huo
kutawezesha kuundwa kwa kikosi maalum cha jeshi la Umoja wa Mataifa
kitakachoweza kuingilia kati katika eneo hilo na kupambana na waasi pamoja na
kuanzisha juhudi mpya za kisiasa.
Viongozi walioutia saini
mkataba huo mjini Addis Ababa ni wa Msumbiji, Rwanda, Tanzania, Afrika Kusini,
Congo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Sudan ya Kusini.
Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Ban Ki-moon pia alikuwapo kwenye hafla ya kutiwa siani kwa mkataba
huo.
Msemaji wa Umoja wa
Mataifa,Nesirky ameeleza kuwa Umoja wa Afrika, mataifa 11 ya eneo la maziwa
makuu, (ICGLR)pamoja na jumuiya ya wanachama 14 ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika (SADC),watakuwa wadhamini wenza.
Umoja wa Mataifa unatarajiwa
kumteua mjumbe maalum atakaefuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa
wamesema kuwa hali ya kutokubaliana mwezi Januari ilitokana na wasi wasi juu ya
taratibu, lakini sio kutokana na maudhui ya mkataba.
Jason Stearns,mchambuzi
anaefuatilia masualaya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,mapema mwezi huu
aliyaita makubaliano hayo kuwa ni "hati isioeleweka kabisa."
Alisema makubaliano
hayo,yanalenga katika vipengele vitatu:"kuyazuwia mataifa ya eneo husika
kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi nyingine,kuhimiza kufanyiwa mageuzi
taasisi dhaifu nchini Congo na kuvutia uratibu bora zaidi wa wafadhili na ushiriki
wao.
Eneo la Mashariki mwa Congo
ambalo lina utajiri mkubwa wa madini limevurugwa na makundi kadhaa yenye silaha
katika muda wa miongo miwili iliyopita,huku makundi mapya ya waasi yakizuka
kila mara,baadhi yao yakiungwa mkono na nchi jirani.
Ongezeko la hivi karibuni la
machafuko lilitokea mwaka 2012 na kusababisha kuzuka kwa kundi la waasi la
Machi 23,(M23) ambalo kwa muda liliuteka mji muhimu wa Goma Novemba mwaka jana.
Kundi la M23 lililoundwa na
wapiganaji wa zamani wa kundi la waasi wa kabila la Watutsi ambao hapo awali
waliingizwa katika jeshi rasmi la serikali ya Congo kwa mujibu wa makubaliano
ya amani, wanadai kuwa masharti ya makubaliano hayo hayakutimizwa.
Akizungumza katika utiaji
saini mkataba huo, Rais Jakaya Kikwete alisema hii ni siku ya historia kwa
wananchi wa DRC, majirani zao na enezo
zima la maziwa makuu.
Alisema wananchi wa DRC
wameteseka kwa muda mrefu na sasa wanahitaji amani, wanastahiki kuishi maisha
bora pamoja na kuhakikishiwa usalama wao.
Alisema Tanzania inaahidi
kutekeleza wajibu wake kuhakikisha mkataba huo unafikia malengo yaliyokusudiwa.
Alimpongeza Katibu Mkuu wa
UN,Ban Ki-Moon kwa juhudi kubwa alizochukua kuhakikisha mkataba huo unasainiwa
na DRC kupata amani ya kudumu.
No comments:
Post a Comment