Padri Mushi kuzikwa kesho
Na
Waandishi wetu
SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imetangaza kuzipa ulinzi nyumba zote za ibada
na kusakwa mtandao mzima wa mauaji ya Padri
Evaristus Gabriel Mushi baada ya serikali kuikabidhi kazi hiyo kwa
wapelelezi wa ndani na wa kimataifa.
Imesema
kuwa tangu timu hiyo kuanza kazi tayari idadi ya washukiwa waliokamatwa
kutokana na mauaji hayo imeongezeka ambapo hivi sasa wanahojiwa.
Hatua
hiyo ya serikali imetangazwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais, Mohammed Aboud Mohammed, ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Padri
Mushi, aliuawa kwa risasi juzi asubuhi
wakati akijitayarisha kwenda kuendesha misa katika kanisa Katoliki, Parokia ya
Mtakatifu St. Joseph, Beir El Ras.
Waziri
Aboud alisema serikali imepokea kwa
masikitiko makubwa muendelezo wa matukio ya mauaji ya viongozi wa dini, na
kuwataka viongozi makanisa, waumini wa dini ya kikristo na wananchi kuwa
watulivu kwani serikali itatumia wapelelezi wa kimataifa kuunasa mtandao wote
uliohusika na mauaji hayo.
Alisema
serikali imeamua kutumia wataalamu hao kwa vile kiwango chao cha upelelezi ni
cha hali ya juu katika matukio ya mauaji.
Alisema
wapelelezi hao wanatarajiwa kuendesha uchunguzi huo katika maeneo mbali mbali
ya visiwa vya Zanzibar
zikiwemo bandari bubu baada ya kuonekana ni moja ya maeneo ambayo hupenda
kutumiwa na wahalifu wa matukio hayo.
Hata
hivyo, alifahamisha kuwa serikali haitataja wapelezi hao walipotoka lakini
tayari wameanza kukamata watu zaidi ambao wanaendelea kufanyiwa mahojiano.
Alisema
serikali imedhamiria kuzika mtandao huo baada ya kuonekana vitendo hivyo
vinaongezeka na kuenea katika jamii jambo ambalo limekuwa likiwatia hofu
wananchi na viongozi wa dini.
Akifafanua zaidi alisema vipo vikundi vya watu
ambavyo lengo lao kubwa kuona kwamba wananchi wa Zanzibar wanaingia katika chuki za kidini.
Alisema
chuki hizo ni pamoja na kuchoma makanisa na kuwaua viongozi wa dini na kuifanya
Zanzibar kuwa
haitawaliki tena katika misingi ya sheria na imani za dini.
Alisema
wakati serikali ikilifanyia kazi suala hilo
ni vyema kwa waumini wa dini kuona wanakuwa watulivu ili kuhakikisha amani ya
nchi inaendelea kudumishwa.
Aidha,
aliwataka wageni na wawekezaji kuendelea kuja nchini kwani mazingira ya Zanzibar bado yako salama
na hakuna mtu ataeweza kudhuriwa.
Alisema
tayari kuna watu wamekamatwa wakiwa na silaha katika bandari bubu ya Nungwi wilaya
ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Wakati huo huo akizungumza na waandishi wa
habari, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Zanzibar, Mhashamu Augostino
Shao amesema Padri Mushi atazikwa
kesho katika makaburi ya Kitope.
Alisema
ibada ya mazishi itafanyika katika
kanisa katoliki la Minara miwili Shangani mjini Zanzibar.
Alisema
Padri Mushi analazimika kuzikwa Zanzibar
kwa mujibu wa sheria za kanisa zinavyoelekeza.
Shao
alisema sheria hizo zinaelekeza kuwa Padri na mali
zake ni mali ya kanisa na sio familia hivyo ndio sababu ya marehemu
Padri Mushi kuzikwa Zanzibar
na sio Moshi nyumbani kwao.
“ Padri
Mushi amekaa Zanzibar tangu ana miaka 18, Upadri kapewa katika Jimbo la
Zanzibar ambalo lina madaraka kamili halitegemei jimbo jengine hivyo anapaswa
kuzikwa hapa alipokuwa akiwatumikia waumini wake na si pengine popote,” alifafanua.
Alisema
Kanisa tayari limeshajitayarisha kwa maziko hayo ambayo yatahudhuriwa na waumini wa kanisa hilo na makanisa mengine,
viongozi mbali mbali wa ndani na nje ya nchi huku likizingatia suala zima la
usalama kwa kushirikiana na vyombo husika.
Akizungumzia
kuhusu hali iliyopo hivi sasa visiwani Zanzibar, Askofu Shao alisema matukio ya
kihalifu yanayotokea anaamini kuwa ni mbinu zinazopangwa nje ya Zanzibar kwa vile Wakristo na Waislamu wa Zanzibar kwa miaka mingi
wamekua wakiishi kwa kusikilizana na kusaidiana bila ya kujua tofauti za dini
zao.
“ Haya
yanayotokea ni dhahiri kuwa yamepangwa nje ya nchi kwani wenzetu hawafurahi
kusikia Tanzania ni nchi ya amani ndio maana wanaamua kufanya kila jambo
kuhakikisha kuwa tunaingia katika mfarakano wa wenyewe kwa wenyewe,” alieleza
Shao.
Alisema
ni vyema vyombo husika vikawajibika ipasavyo katika majukumu yao
ya kazi kwa lengo la kuliondoa tatizo hilo.
Aidha
alisema tatizo sio uislamu wala ukristo tatizo ni suala la kuwadhibiti wahalifu
kwani katika dini yoyote wapo wahalifu hivyo ni vyema vyombo husika vikaacha
kufanya kazi kwa kujuana.
Askofu
Shao akizungumzia suala la kuletwa wataalamu wa masuala ya uchunguzi kutoka nje
ya nchi alisema suala hilo
haliafiki kwa sababu nchi inapofikia hatua ya kutaka msaada kutoka nje ni dhahiri
kuwa haina usalama jambo ambalo linaweza kusababisha kuwekewa vikwazo mbali
mbali ikiwemo misaada na vikwazo vya kiuchumi.
Aidha
aliitaka serikali kuhakikisha wahalifu wa matukio mbali mbali wanakamatwa na
kuchukuliwa hatua za kisheria bila ya kujali nani alihusika katika matukio
hayo.
Alikielezea
kifo cha marehemu Mushi, alisema ni pengo kubwa katika kanisa hilo
ambapo yeye alikuwa akijishungulisha zaidi na masuala ya kukuza maendeleo elimu
katika kanisa hilo.
Akielezea
jinsi alivyopokea taarifa ya kifo cha msaidizi wake mkuu,Shao alisema wakati
alipokuwa akiendesha ibada ya kawaida ya Jumapili hapo kanisa la minara miwili
akiwa katikati ya ibada hiyo alipokea taarifa ya kifo cha marehemu Mushi.
“Unajuwa mimi nilikuwa naongoza ibada lakini
wenzangu tayari walikuwa wamepata taarifa ya kifo cha marehemu Mushi,ambaye
nilikuwa naye asubuhi saa 12:00 tukiagana yeye akielekea kuongoza misa huko
Mtoni katika kanisa liliopo eneo la Beit-el-Ras,” alisema.
Askofu
Shao akifafanua matukio ya hujuma kwa viongozi wa dini ya kikristo alisema hivi
sasa uvumilivu wa kidini Zanzibar umeanza kutoweka kidogo kidogo, tofauti na
miaka ya nyuma ambapo Zanzibar ilikuwa ikisifika
kuwa kisiwa chenye watu wenye dini tofauti wanaoishi pamoja kama
ndugu huku wakipendana.
Alisema
wapo watu wenye dhana kwamba Zanzibar
iwe nchi ya kiislamu na kuongeza kwamba watu hao wanakosea sana kwa sababu hata
huo mji mtakatifu wa makka wapo waumini wa madhehebu mbali mbali ambao
wanaishi kwa kuheshimiwa kwa mujibu wa imani zao.
Aliwataka
wananchi kutumia mchakato wa mabadiliko ya katiba kutoa maoni yao kwa uwazi na uhuru huku wakibainisha
mambo ambayo wanaona ni kero kwao.
Aidha,
Shao, alivitaka vyombo vya ulinzi kufanya kazi za kuwasaka wahalifu kwani jamii
wa wakristo tayari wameanza kupoteza imani kwa taasisi hizo.
Kwa
upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein, ameelezea kupokea kwa mshtuko mkunwa mauaji ya Padri Evaristitus
Mushi na kutoa pole kwa waumini, ndugu jamaa, marafiki na wananchi
wote wa Zanzibar kufuatia kifo hicho.
Katika
taarifa yake kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed
Aboud, Dk. Shein alisema serikali kwa
kushirikiana na jeshi la polisi itawasaka hadi kuwatia mikononi na hatimaye
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na mauaji hayo.
Hapo
jana Dk. Shein alikutana na Askofu Shao katika Ikulu ndogo Migombani na kueleza
masikitiko yake kutokana na kifo hicho cha ghafla cha Padri Mushi na kuelezea
haja ya kuwepo kwa uvumilivu katika kipindi hichi cha msiba.
Habari
hii imeandikwa na Mwantanga Ame, Haroub Hussein na Rajab Mkasaba, Ikulu
Naomba kama kuna mwenye taarifa atueleze ivi imekuwaje wale waliompiga risasi yule liongozi wa kanisa siku za nyuma na wale waliomwagia tindikali Ust Soraga? Nakumbuka kulitumwa kikosi maalum kuchunguza matukio yale.Au ilikuwa danganya toto?
ReplyDeleteKatika kesi ya padri aliyepigwa risasi mpendae, kuna watu tuliambiwa wamekamatwa na wanahojiwa. Hofu yetu ni kuwa hatujui kama bado wapo ndani au la. Ni bora serikali na vyombo vya sheria vikawa wazi katika maswala haya. kesi ziwe open na kila hatua ijulikane. serikali na vyombo vyake hatuviamini vizuri wanaweza wakadhalilisha watu kwa visingizio vya uongo.
ReplyDelete