Habari za Punde

Watu watatu wafariki Micheweni



Na Masanja Mabula,Pemba
WATU watatu wamefariki dunia kwenye matukio mawili tofauti yaliyotokea katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba likiwemo na watoto wawili kuzama baharini wakati wakitoka kuchukua kuni katika bahari ya Pondeani Kinowe.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Sadi alisema katika tukio hilo lililotokea siku ya Jumapili watoto hao wakiwa na wenzao sita waliondoka nyumbani kwao kwa ajili ya kwenda kuokota kuni wakiwa na chombo aina ya dau.

Aliwataja waliokufa maji kwenye tukio hilo kuwa ni Hamad Mwinyi Hamad (10) ambaye tayari amezikwa pamoja na Ali Mwinyi Hamad (6) ambaye bado hajaonekana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.


Aidha kamanda Sadi amewataja walionusurika kufa kuwa ni Mohammed Hamad Mohammed (10) , Rashid Juma Rashid (10) Ali Juma Rashid (8)  Rashid Mansour Rajab (10) Suleiman Mwalim  Mkongwe (8) pamoja na nahodha wa chombo hicho Rajab Mansour Rajab (26).

Aidha aliwataka wazazi kuwa na uangalifu na udhibiti wa watoto wakati wanapotaka kwenda baharini ikiwa ni kufuatana na watu wazima zaidi ya watatu ili kuweza kukinga na maafa yanayoweza kuzuilika.

Kwa upande wake sheha wa Shehia ya Tumbe Mashariki, Seif Omar alisema  tayari  kijana Hamad Mwinyi Hamad ameshazikwa na kwa sasa wanendelea kuutafuta mwili wa Ali Mwinyi Hamad kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

"Boti za wavuvi wa Tumbe , wananchi wa Tumbe  kwa kushirikiana na jeshi la polisi wanaendelea kuutafuta mwili wa Ali Mwinyi Hamad katika bahari za Tumbe," alieleza .

Na katika tukio jengine mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 55 mkaazi wa kijiji cha Chamboni  shehia ya Micheweni anayefahamika kwa jina la Bihaba Omar Juma amefariki dunia baada ya kuangukiwa na jiwe wakati akiokota mawe kwa ajili ya kutengeza kokoto.

Tukio hilo limetokea Jumapili majira ya saa tano za asubuhi  wakati mwanamke huyo akiwa katika harakati zake za kujitafutia riziki, na akichukua mawe kwenye machimbo ya mawe huko Micheweni jiwe kubwa lilimwangukia na kusababisha kifo chake.

Matukio ya watu kuangukiwa na mawe na kisha kufariki dunia yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika machimbo ya mawe Micheweni na kusababisha vifo vya watu mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.