Wizara tano kushughulikia
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameziagiza Wizara tano za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukaa pamoja kuhakikisha kuwa inazitafutia ufumbuzi tatizo la kuingia maji ya bahari katika mashamba ya mpunga ya Bonde la Koowe katika kijiji Njuguni, Shehia ya Njuguni, wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Wizara hizo ni Wizara ya Kilimo na Maliasili, Uvuvi na Mifugo, Miundombinu, Uwezeshaji, Ofisi za Makamu wa Kwanza wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Rais alitoa agizo hilo mara baada ya kukagua na kupokea taarifa ya ujenzi wa tuta la kuzuia maji ya bahari kuingia katika mashamba hayo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dk. Islam Seif Salum.
Katika maelezo yake kwa Rais, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema mradi huo wa ujenzi wa tuta lenye urefu wa mita 1700 ulioanza mwaka 2009 unahitaji shilingi milioni 260 ambapo hadi sasa zimetumika shilingi milioni 84.9 lakini alionyesha wasiwasi kuwa fedha hizo hazipo kwa wakati huu.
Hivyo Dk. Shein alizitaka wizara hizo zikae pamoja na kuangalia kwanza namna zitakavyochangia kupata fedha hizo kumaliza mradi na pili kuangalia kitaalamu zaidi namna ya kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo uwezekano wa baadhi ya mashamba yanayoathirika kugeuzwa kuwa mabwawa ya kufugia samaki.
“Tusisubiri wafadhili katika hili. Mradi huu unahusisha wizara nyingi hivyo ufumbuzi wale uchukue sura hiyo hivyo nawaagiza viongozi wa wizara za Kilimo, Wizara ya Uvuvi, Wizara ya Miundombinu, Wizara ya Uwezeshaji, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa maana ya mhusika wa mazingira na Ofisi ya Makamu wa Pili kwa maana ya TASAF mkae pamoja mlimalize”alisisitiza.
Dk. Shein aliwaambia wananchi wa Njuguni kuwa serikali yake inafanya jitihada zote ili suluhisho la tatizo hilo lipatikane kabla ya mwisho wa mwaka huu na kuwahimiza kuendelea kushirikiana na serikali katika kufanikisha jambo hilo.
“Tumekuja hapa kuangalia nini cha kufanya na tunatafakari zaidi namna ya kumaliza tatizo hili. Tunataka maendeleo ya kilimo cha mpunga na pia tunafikiria ufugaji wa samaki” alisema.
Hata hivyo aliwakumbusha wananchi hao kuwa tatizo hilo linatokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameathiri sehemu nyingi za visiwa vya Unguja na Pemba na kueleza kuwa mabadiliko hayo yamechangiwa pia na ukataji wa miti ya mikoko katika maeneo yao.
Kwa hiyo aliwaeleza moja ya jitihada za serikali ni kupanda miti hiyo tena katika eneo linalopatakana na mashamba yao.
Awali akitoa ripoti ya mradi huo Naibu Katibu Dk. Islam alisema kuna jumla ya maeneo 148 katika visiwa vya Unguja na Pemba yaliyoathirika na mabadiliko na tabianchi ambapo sasa maji ya bahari yamevamia maeneo hayo.
Katika bonde hilo la Koowe lenye ekari 170 na wakulima wapatao 360 alieleza Dk. Islam kuwa jitihada za kukabiliana na hali hiyo zilianza kwa kupanda miti lakini hazikufanikiwa kutokana na wananchi kupanda miti isiyostahiki hivyo upandaji miti utaanza tena kwa kupanda miti sahihi kwa eneo hilo.
Rais ambaye yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya siku sita kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi anaendelea na ziara katika Mkoa wa Kaskazini Pemba katika Wilaya ya Wete.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na Mawaziri na watendaji wakuu wa wizara mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayojitokeza wakati wa ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment