Habari za Punde

Dk. Shein:Acheni kugombania misikiti


Rajab Mkasaba, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohamed Shein amewaasa waumini wa dini ya kiislamu kutoanzisha mizozo kwenye misikiti kwa kugombania uongozi.

Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa msikiti wa masjid Imran uliopo kijiji cha Fimbo na Mkadini shehia ya Kigongoni Kiuyu, jimbo la Ole mkoa wa Kaskazini Pemba.

Dk. Shein alisema miongoni mwa waumini hao watapatikana maimamu na maamuma, hivyo ipo haja ya kuridhika na wale wote watakaobahatika kuwa maimamu.

“Tuzitekeleze taratibu za dini yetu ya kuwapata viongozi… tuendeleze ibada kwa njia ya maelewano na mafahamiano,” alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, aliwataka waumini wa dini hiyo kuzidi kupendana na kuombeana mema pamoja na kushikamana bila ya kufarakana kwani umoja wao ndio utakaowawezesha kuendelea kuishi kwa amani.

Alisisitiza kuwa elimu ya dini ni muhimu hasa katika enzi hizi ambazo kumezuka mambo mengi katika jamii ambayo yanahitaji elimu.

Aliwataka waumini wazidi kuitumia misikiti kuwa ni vituo vya elimu ya dini.
Dk. Shein alitoa wito kwa wazazi na walezi kutokana na mnasaba wa kuwepo misikiti mingi wawanasihi vijana kwenda misikitini na kujifunza dini ya kiislamu na maadili mema.

Alisema ujenzi wa misikiti ni ishara njema ya kuimarika imani ya waislamu na kufuata mwenendo wa Mtume (SAW) ambaye hatua yake ya mwanzo baada ya kutoka Makka kabla ya kujenga msikiti wa Madina alijenga msikiti Qubbah.

Alieleza kuwa misikiti hiyo inayojengwa ni nyumba za ibada, na vile vile ni mwahala mwa kueneza nuru ya Uislamu ambayo chanzo chake kikubwa ni elimu ya dini na maisha mema, hivyo ipo haja ya kuitumia vyema.

Wananchi na waumini wa kijiji hicho katika risala yao, walieleza kufarajika kwao kwa jinsi Dk. Shein anavyojali na kuthamini juhudi za maendeleo ya wananchi wake.

Walisema changamoto zinazowakabili ni barabara na huduma ya umeme changamoto ambazo Dk. Shein aliahidi kuzipatia ufumbuzi.

Ujenzi wa msikiti huo umegharimu shilingi milioni 80 fedha ambazo zinatokana na michango ya wanakijiji na wananchi mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.