Habari za Punde

Makachero wajifungia kumaliza uhalifu


Na Mwandishi wetu, DSM
WAKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI’s) kutoka Umoja wa Wakuu wa Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO)leo wanaanza mkutano wa siku mbili jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa jeshi la Polisi, Advera Senso amesema mkutano huo wa siku mbili utafunguliwa na Mwenyekiti wa sasa wa SARPCCO ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Said Mwema.

Alisema katika mkutano huo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya operesheni za pamoja na ushirikiano baina ya SARPCCO na umoja wa wakuu wa Polisi wa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO).

Alisema mkutano huo pia utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na wakuu wa Polisi wa SARPCCO katika mkutano uliofanyika Zanzibar Septemba mwaka jana.

Aidha alisema kamati tendaji za SARPCCO ambazo zinajumuisha wajumbe kutoka nchi wanachama katika nyanja za sheria, mafunzo na kamati tendaji inayoshugulikia mambo ya wanawake na jinsia zitajadiliana ili kutoka na maazimio ambayo yatapelekwa katika mkutano wa wakuu wa Polisi utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu.

Tayari wajumbe wa mkutano huo wameanza kuwasili jijini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.