Habari za Punde

MOAT, Wadau Kukutana na Vyombo vya Usalama


Na Fatma Kitima,DSM
WADAU wa habari wakishirikiana na chama cha wamiliki wa vyombo vya habari nchini (MOAT) watakutana na taasisi za ulinzi na usalama kujadili kwa kina sababu za kushambuliwa waandishi wa habari pamoja na wanaharakati wengine.

Mbali ya taasisi za ulinzi na usalama, wadau hao pia watakutana na Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Dk. Edward Hossea.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam, wadau hao wamesema wameundana Kamati ya watu 16, ambayo ndiyo iliyopewa jukumu hilo.

Kamati hiyo itakutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa jeshi la Polisi, IGP Said Mwema, Mkuu wa Usalamawa Taifa, Othman Rashid na TAKUKURU.

Hatua hiyo imekuja baada ya tukio la kinyama la kushambuliwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Absolon Kibanda.

Wadau hao walisema shambulizi dhidi ya Kibanda ni shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na kuwajengea hofu wahariri, waandishi na wanaharakati ili wasitekeleze wajibu wao kwa umma.

Walisema tukio hilo ni mfululizo wa mashambulizi ya wanahabari na wanaharakati na kusema katika mazingira hayo wamegundua hakuna aliye salama.

Walisema matukio ya kushambuliwa Mhariri wa gazeti la Mwanahalisi, Said Kubenea, kutekwa kwa Dk. Steven Ulimboka, kuuawa mwandishi wa habari wa Chanel Ten, Daud Mwangosi na kushambuliwa Kibanda inasababisha kuzorota utendaji wa wanahabari na wanaharakati.

Aidha wadau hao wameelezea kusikitishwa na kile walichodai baadhi ya maafisa wa usalama kutumiwa kutekeleza vitendo vya uhalifu ambavyo ni tishio kwa usalama wa waandishi wa habari.

Wameiomba serikali iunde tume huru kuchunguza kwa undani matatizo hayo na kudai kasi ya uchunguzi wa vyombo vya usalama hairidhishi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.