Na Husna Mohammed
WAJAWAZITO 38 walifariki mwaka jana katika hospitali kuu ya Mnazimmoja kutokana na matatizo mbalimbali ya uzazi.
Aidha katika kipindi cha mwaka 2011 jumla ya kesi 52 za vifo vinavyotokana na matatizo hayo ya uzazi zilitokea hospitalini hapo.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mnazimmoja, Daktari dhamana wa wodi ya wazazi, Mwana Omar, alisema kesi hizo za vizazi ni zile zilizoripotiwa katika hospitali hiyo.
“Kesi hizi za vifo vya mama wajawazito ni zote zinazoripotiwa hapa iwe za uhamisho kutoka katika hospitali au vituo vya afya vyengine au hata mimba zisizotimia zote zinatokana na matatizo ya uzazi,” alisema.
Alisema katika kipindi cha mwaka jana jumla ya akinamama wajawazito 11,050 walilazwa hospitalini hapo ambapo kati ya hao 11, 013 walijifungua, na akinamama 1,667 walijifungua kwa njia ya upasuaji na 9346 walijifungua kwa njia ya kawaida.
Pia katika kipindi cha mwaka 2011 akinamama wajawazito 10,907 waliripoti na kulazwa katika hospitali hiyo kutokana na matatizo mbalimbali ya uzazi ambapo kati ya hao 10,782 walijifungua kati ya hao 1,704 walifanyiwa upasuaji na 9,078 walijifungua kwa njia ya kawaida.
Dk. Mwana alisema kesi nyingi za vifo kwa wazazi wanaoripoti katika hospitali hiyo zinatokana na kumwagika kwa damu nyingi wakati wa ujauzito au hata katika kipindi cha kujifungua.
Sambamba na hilo alisema pia kifafa cha mimba kwa akinamama katika kipindi hicho cha ujauzito na hata wakati wa kujifungua kimekuwa kikisababisha vifo vya akinamama wajawazito.
Alifahamisha kuwa matatizo yatokanayo na uzazi yamekuwa yakichangiwa ukaribu na ukosaji wa taaluma kwa mama wajawazito.
“Akinamama wajawazito wengi wanakosa taaluma ya kwenda kliniki na mapema kwa ajili ya kujua vidokezo vya hatari na hivyo kuchukua tahadhari katika kipindi cha ujauzito ambapo matatizo mengine yanaweza kuepukika,” alisema.
Aidha Dk. Mwana alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakipuuza ushauri wa wakunga jambo ambalo linachangia matatizo na hata vifo.
Hata hivyo, alisema huduma za afya za mama wajawazito zimeimarika katika hospitali na vituo vya afya jambo ambalo linatia faraja kwa huduma hizo.
Akizungumzia vifaa katika wodi ya wazazi, Dk. Mwana alisema vifaa hivyo vimekuwa vikipatikana hospitali mbalimbali zenye kushughulika na mambo ya uzazi hata kama vinachelewa kidogo baadhi ya siku lakini vinapatikana.
Alisema wodi hiyo ya wazazi inakabiliwa na tatizo kubwa la manesi wa uzalishaji ukilinganisha na wingi wa wazazi wanaoripoti katika hospitali hiyo.
Aidha mwandishi wa habari hizi alishuhudia wimbi la wazazi waliofika katika hospitali hiyo ambapo kitanda kimoja kilikuwa na wazazi watatu hadi wanne na wengine wakiwa chini katika magodoro jambo ambalo halipendezi kwa afya ya wazazi.
Kwa upande wa akinamama wajawazito na wale waliojifungua katika hospitali hiyo ambao walilazwa jana na kufanya mahojiano na gazeti hili, walikiri kuwa huduma za uzazi wamekuwa wakipata bure na kwamba ni mambo madogo tu ndio wanaochangia kama hayapatikani kwa muda huo.
Arafa Hassan (28), mkaazi wa Bububu, ambae alijifungua kwa njia ya upasuaji alisema alichangia dawa na plasta baada ya kukosekana kwa wakati huo.
“Nimechangia hata shilingi 10,000 hazifiki baada ya kuambiwa nifanye hivyo ambapo kwa wakati huo vilikosekana vifaa hivyo,” alisema.
Nae Zawadi Bahati, mkaazi wa Mwera ambae alijifungua kwa njia ya kawaida alisema hadi sasa hajatakiwa kuchangia chochote.
Maryam Shauri Mkombe, ambae ni nesi wa wodi ya wazazi, alisema wazazi hawalazimiki kuchangia kifaa hata kimoja labda pale ambapo havijafika kwa wakati huo.
No comments:
Post a Comment