Habari za Punde

JK akiri Upungufu Wataalamu Hakimiliki

Na Kunze Mswanyama,DSM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Jakaya Mrisho Kikwete amekiri kuwepo upungufu mkubwa wa wataalamu wa kudhibiti hakimiliki za wagunduzi na wabunifu wa bidhaa nchini.

Hivyo amekiagiza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),kuhakikisha kinaanzisha shahada ya uzamivu katika fani hiyo ili kuongeza idadi ya wataalamu hao.

Pia aliwataka wazalishaji wadogo na wa kati kuhakikisha wanasajili bidhaa zao walizogundua kwa wakala wa usajili wa alama za biashara na makampuni (BRELLA) ili kukuza pato binafsi na la taifa (GDP).

Rais Kikwete aliyasema hayo jana alipofungua mkutano wa kimataifa wa kujadili mafanikio na changamoto za kazi za wagunduzi na wabunifu katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani,elektroniki na hati miliki,ulioandaliwa na Taasisi ya WIPO unaoendelea jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha Mawaziri zaidi ya 20 wa nchi mbalimbali.

Aliwaagiza wabunifu wote kuhakikisha wanalinda kazi na bidhaa zao ili kujipatia uhakika wa kipato lakini pia wakijitahidi kupambana ili kuongeza idadi ya bidhaa za Tanzania zinazoingia kwenye soko la kimataifa.

“Nawasihi wakulima wa zao la kahawa,kuanza kuangalia utaratibu wa kusajili na kuweka nembo ya ubora katika bidhaa zenu ili kuongeza nguvu kwenye soko na nina mfano mmoja wa Ethiopia ambao wameanza kufaidika zaidi kwa kuweka alama kwenye kahawa yao inayouzwa dunia nzima,” alisema.

Alisema inawezekana kabisa kwa nchi kujipatia zaidi ya asilimia tano ya pato la taifa kutokana na uuzaji wa bidhaa zenye nembo ya usajili wa Tanzania na kuliagiza shirika la viwango nchini (TBS),kuacha urasimu linapotakiwa kutoka usajili wa ubora wa bidhaa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WIPO,Francis Gurry,alisemakama itatumika vizuri,njia hiyo inaweza kupunguza umasikini na kuzidisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

Alisema ubunifu ndio msingi wa ukuaji wa kiuchumi,maendeleo na kazi bora pia ni ufunguo wa makampuni kushindana kiukamilifu katika soko la dunia ambalo linahitaji bidhaa zenye ubora na zenye kuonesha zinapotoka jambo ambalo nchi nyingi za kiafrika hazijafikia.

Kwa upande wake Toshikiro Kose,Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Alama,Ubunifu na Utawala katika Wizara ya Uchumi,Viwanda na Biashara ya nchini Japan,alisema nchi yake imejitolea kwa hali na mali kutoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha nchi za kiafrika zinafaidika na kazi za ubunifu kama ambavyo nchi yake inafaidika na kazi zao.

Awali Waziri wa Viwanda na Biashara Dk.Abdallah Kigoda,alisema ni lazima sheria za kuwalinda wagunduzi na wabunifu kuboreshwa zaidi ili kuhakikisha kila mmoja anafaidika na alichokigundua.

Mkutano huo unaowahusisha mawaziri toka nchi 20 wanaohusika na sayansi na teknolojia,Biashara,wakuu wa vituo vya ugunduzi, makampuni makubwa ya Afrika, Jumuiya za kiuchumi na maofisa waandamizi wa serikali,umeandaliwa na WIPO,Umoja wa Matifa kupitia Baraza la Uchumi (ECOSOC) na serikali ya Tanzania.

Mkutano huo unatarajiwa kuhitimishwa siku ya jumatano ambapo pamoja na mambo mengine Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania,Mizengo Pinda atahutubia na kuufunga rasmi huku maazimio kadhaa yakipelekwa serikalini kwa hatua zaidi.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.