Habari za Punde

Dk.Shein:Marufuku Vigogo kupewa Nyumba za Maendeleo

Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohamed Shein, amemuagiza Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, kuhakikisha nyumba za maendeleo Mpapa, haziingii mikononi mwa vigogo na badala yake wapatiwe wananchi wenye shida ya makazi.

Dk. Shein, aliyasema hayo wakati akifanya majumuisho ya ziara yake katika mkoa wa kusini Unguja, Chuo Kikuu cha Zanzibar, kilichopo Tunguu.

Dk. Shein, alisema dhamira ya serikali kujenga nyumba za maendeleo ni kuona wananchi wanapata makaazi bora,lakini jambo la kusikitisha wananchi hao hawapatiwi badala yake hugawiwa vigogo.

Alisema kuna baadhi ya watu hivi sasa wamekuwa wakiishi mijini na wanamiliki nyumba zaidi ya mbili, lakini jambo la kusikitisha wanatumia vibaya mamlaka yao kwa kupeleka maombi ya kupatiwa nyumba hizo.

Alisema serikali haitakubali kuona hilo linatokea tena na kumtaka waziri mwenye dhamana ya makazi kuhakikisha nyumba hizo wanapewa watu wenye mahitaji.

“Nina taarifa hivi sasa kuna maombi 1,000 ya watu ambao wanataka kupewa nyumba za maendeleo za Mpapa, nakuagiza waziri uwape wenye mahitaji sio kuwapa wakubwa,”alisema.

Alisema uwezo wa serikali kujenga nyumba za aina hiyo umepungua kwa kiasi kikubwa kiasi ambacho haiwezi kujenga nyumba mpya lakini inachofanya ni kuzimalizia zile zilizoachwa na Mzee Karume.

Alisema serikali itazifanyia matengenezo nyumba za maendeleo Kengeja Mkoani, Chake Chake na Mtemani Wete kisiwani Pemba.

Akizungumzia sekta ya elimu, Dk. Shein, aliwataka viongozi wa mkoa huo, kuhakikisha watoto wote waliotoroka skuli wanarejeshwa madarasani, kuendelea na masomo yao.

Alisema ni lazima viongozi wa mkoa walishughulikie hilo kutokana na kuonekana tatizo hilo linaanza kukua, baada ya taarifa za Mkoa kueleza kuwa utoro katika skuli za msingi umefikia asilimia 6 huku sekondari ikifikia asilimia 7.

Dk. Shein, aliuagiza uongozi wa mkoa huo kuanzisha chuo cha amali, ili kuweza kuwasaidia vijana kujifunza stadi za maisha ili wajiajiri badala ya kutegemea chuo cha Amali cha Mkokotoni pekee.

Kuhusu kilimo, alisema bado serikali ina dhamira ya kuendeleza kazi hizo kwa kupitia miradi mbali mbali ya kilimo cha umwagiliaji maji na tayari inafanya mazungumzo na serikali ya Japan huku serikali za Marekani na Vietnam zikiwa zimekubali kusaidia sekta hiyo.

Akigusia huduma ya maji, alisema dhamira ya serikali ni kuona inakuza kiwango cha upatikanaji maji nchini kupitia miradi mbali mbali ambayo inaendelea kutekelezwa.

Hata hivyo, Dk. Shein, ameionya jamii kuacha tabia ya kujiungia maji kiholela au kwa kutumia mabomba makubwa ambayo huwafanya wengine kukosa huduma hiyo.

Akizungumzia juu migogoro ya ardhi, Dk. Shein, aliwapongeza viongozi wa mkoa huo kwa kufanikisha kutatua baadhi ya migogoro ukiwemo wa Mchangamle, na kuanzia sasa wasiruhusu kutokea kwa matatizo ya aina hiyo.

Aidha, Dk. Shein, aliwataka viongozi kote nchini kutumia nafasi zao kwa kufanya kazi za kujitolea ikiwa ni hatua itakayoweza kurejesha moyo wa kufanya kazi vizuri.
Aidha aliwataka kuwa karibu na wananchi badala ya kuendeleza mtindo wa sasa wa kuwakimbia.

Katika ziara huyo Dk. Shein, alifungua mradi wa maji safi na salama wa kijiji cha Chwaka, kukagua mradi kama huo Machui, kutembelea ujenzi wa nyumba za maendeleo Mpapa, kilimo cha mpunga Muyuni na mradi wa ujenzi jengo la wanamazingira Jambiani, ambapo aliendesha harambee na kukusanya shilingi milioni 24 ambapo yeye binafsi alichangia shilingi milioni 10.

Wakati huo huo Rajab Mkasaba anaripoti kuwa Dk. Shein ameeleza kuwa azma ya serikali ni kuhakikisha inajitegemea katika upatikanaji wa dawa.

Dk. Shein aliyasema hayo baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha afya Kajengwa Makunduchi kilichojenwga na wananchi.

Alisema nia ya serikali ni wananchi kutolipia ada katika huduma ya afya bali kubwa linalofanywa ni kuchangia tu huduma hiyo.

Alitoa pongezi kwa wananchi na wanakijiji kwa uamuzi wao wa kujenga kituo hicho na kuwaahidi uwa nia ya serikali ni kuhakikisha Cottage ya Makunduchi inakuwa ya mwanzo kuwa hospitali ya wilaya.

Mapema Dk. Shein akizingumza na wananchi na wakulima wa bonde la mpunga la Muyuni katika skuli ya Muyuni, alisema serikali imeamua kuwasaidia wakulima na itaendelea na azma yake hiyo.

Alisema serikali itaendelea kuwasaidia wakulima kwa kuwapa mbolea, dawa za kuulia magugu, mbegu bora kwa bei nafuu ili waweze kulima kwa uhakika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.