Habari za Punde

Wauza samaki Feri waulalamikia uongozi

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwasili katika soko la samaki la Feri Dar es Salaam, kuangalia harakati za biashara katika soko hilo
 Katibu wa umoja wa wakusanyaji na wauzaji wa samaki katika soko la Feri, Khamis Said Suleiman akitoa dukuduku lake kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipofanya ziara ya kutembelea soko hilo jana
 Meneja wa soko la samaki Feri, Charles Kapongo akitoa ufafanuzi mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kuhusiana na mzozo uliopo baina ya uongozi wa soko hilo na wauzaji samaki, wakati alipotembelea soko hilo jana
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akijuilia wagonjwa katika hospitali ya Amana Dar es Salaam, wakati alipofanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo jana . (Picha na Salmin Said, OMKR).

Na Hassan Hamad OMKR
 
Umoja wa wakusanyaji na wauzaji samaki wa soko la Feri Dar es Salaam, wameulalamikia uongozi wa soko hilo kwa madai ya kunyimwa uhuru wa kufanya shughuli zao katika soko hilo.
 
Katibu wa umoja huo bw. Khamis Said Suleiman ametoa malalamiko hayo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipofanya ziara ya kutembelea soko hilo.
 
Amesema tokea lilipofunguliwa soko hilo mwaka 2002 wamekuwa wakifanya shughuli zao bila usumbufu, lakini tangu soko hilo likabidhiwe kwa mkandarasi hivi karibuni, wamekuwa wakinyanyasika kwa kutopewa fursa ya kutosha ya kufanya shughuli zao.


Amesema umoja huo upo kisheria na umekuwa ukiendesha shughuli zake kwa kufuata taratibu zilizowekwa, lakini kwa sasa wameshangazwa na hatua ya kuwekewa vikwazo wasivyovielewa, na kusababisha samaki kadhaa kuharibika.
 
Akitoa ufafanuzi juu ya kadhia hiyo, meneja wa soko hilo bw.Charles Kapongo amekiri kuwepo kwa usumbufu huo kwa wauzaji wa samaki tangu soko hilo akabidhiwe mkandarasi.
 
Bw. Kapongo amefahamisha kuwa baada ya mkandarasi huyo anayehusika na ukusanyaji wa taka na ushuru kukabidhiwa soko hilo, watendaji wa Manispaa ya Ilala walikaa kutathmini hali ya ukusanyaji wa mapato na kubaini kuwepo kwa upotevu mkubwa wa fedha unaotokana na ukusanyaji mbaya wa mapato.
 
Amesema kufuatia hali hiyo Manispaa iliamua kutoza asilimia tano ya mauzo lakini wakusanyaji na wauzaji hao wa samaki wamekuwa wakiingiza samaki kwa makontena na kusababisha kukosekana kwa thamani halisi ya samaki hao na ushuru unaotakiwa.
 
Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewashauri wafanyabiashara hao kuwasilisha malalamiko yao kwa taasisi zinazohusika, na kuahidi kushirikiana nao katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
 
Hadi tunatuma taarifa hizi, habari kutoka soko hilo la samaki zinasema bado mivutano inaendelea baina ya uongozi wa soko na wauzaji samaki, jambo ambalo linapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka ili kuruhusu shughuli za biashara ya samaki kuendelea kama kawaida.
 
Wakati huo huo Maalim Seif amefanya ziara ya kutembelea hospitali ya Amana katika manispaa ya Ilala, na kujionea hali ya utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
 
Akiwa katika wodi ya wazazi Maalim Seif amesifu juhudi za madkatari katika kuwahudumia wagonjwa hasa wanaokwenda kujifungua, licha ya kuwepo kwa upungufu wa vifaa vikiwemo vitanda vya kulazia wagonjwa.
 
Hata hivyo amesema juhudi hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya akinamama wanaokwenda kujifungua pamoja na watoto.
 
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF amekamilisha ziara yake katika Wilaya tatu za Mkoa wa Dar es Salaam kwa mkutano wahadhara uliofanyika eneo la Vingunguti reline.
 
Katika mkutano huo amewahimiza wanachama kujitokeza kwa wingi kuomba nafasi za ujumbe wa mabaraza ya katiba, ili mabaraza hayo yaweze kuwa na uwakilishi wa kutosha kutoka chama cha CUF.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.