Na Ali Issa Maelezo Zanzibar 19/3/2013
Imeelezwa kuwa ipo haja ya kufanywa marekebisho ya haraka kwa Sheria ya Magazeti ya Zanzibar ya mwaka 1988 kutokana na sheria hiyo kupitwa na wakati.
Aidha katika zama hizi za uwazi na demokrasia suala la upatikanaji wa habari ni muhimu sana katika kukuza uwajibikaji lakini sheria hiyo ya Magazeti inawanyima watu fursa ya kupata habari hizo.
Hayo yameelezwa na Waandishi wa Vyombo mbali mbali vya habari katika Mkutano wao wa kutoa mapendekezo yanayohusu marekebisho ya Sheria namba 5 ya mwaka 1988 huko katika Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.
Akichangia katika Mkutano huo mmoja wa Washiriki alisema katika sheria hiyo Polisi wamepewa Mamlaka ya kupekuwa katika Chumba chochote cha habari bila kipingamizi chochote kwa kile kinachodaiwa kumtilia mwandishi mashaka.
“Kwa kweli sheria hii inamfanya hata Mwandishi kuwa muoga wa kazi yake maana Polisi kapewa Mamlaka ya kupekuwa hata chumba cha habari iwapo tu atakutuhumu hivyo tunaomba sheria ambayo walau Jeshi la Polisi litafanya upekuzi kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari” Alisema Mwashamba Juma.
Aidha Waandishi hao waliilezea Sheria hiyo kuwa inatoa Mamlaka kupindukia kwa Waziri wa habari na Mkurugenzi wa Habari kufanya maamuzi wanayoyataka bila hata kuwekewa kipingamizi chochote.
“Kwa mujibu wa sheria hii Waziri tu pengine kwa utashi wake bila hata kushirikiana na mtu yeyote anaweza kuamka na kusema Gazeti fulani nimelifungia na ikakubalika kulingana na Mamlaka aliyopewa kisheria” Alisema Ali Bakar.
Waandishi hao pia waligusia kipengele cha adhabu kwa mtu atakayekiuka sheria hiyo nakupendekeza kuwa kunahitajika marekebisho ili iendane na wakati.
“Tunapendekeza adhabu ya kifungo na faini vilingane viwe na uwiano, haiwezekani faini shilingi elfu tano na kifungo miaka mitatu,” alibainisha Miza Kona.
Awali akitoa nasaha zake Kaimu Mkurugezi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Fakih Haji Mbaruok aliwataka Waandishi hao kutoa mawazo yatakayowezesha kupatikana kwa sheria inayokidhi maslahi ya Taifa na wakati uliopo.
Amesema umakini unahitajika kwa waandishi hao ili kupatikana kwa sheria ambayo haitotoa upendeleo au kumkomoa mtu yeyote katika kufanya kazi zake.
“Sheria ni sheria ikipitishwa imepita wandishi tuwe makini kwa kuiangalia sheria hii kwa mapana na kupendekeza maoni yetu kwani sheria kawaida inagusa maisha ya watu na sisi ni wahusika wa moja kwa moja wa sheria hiyo”, alisema Fakih.
Mkutano huo ambao umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ni watatu kufanyika katika kutoa mapendekezo kwa ajili ya marekebisho ya sheria ya namba tano ya magazeti ya mwaka 1988
No comments:
Post a Comment