Habari za Punde

Stars, Morocco zavuna 226.5 m/-

Na Boniface Wambura
 
MECHI ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania, Taifa Stars na Morocco, Simba wa Atlas iliyochezwa juzi uwanja wa Taifa Dar es Salaam, imeingiza shilingi milioni 226, laki tano na elfu 46.
 
Katika mechi hiyo, Tanzania iliibuka na ushindi maridhawa wa mabao 3-1.
 
Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 32,614 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha shilingi 5,000, 7,000, 10,000, 15,000, 20,000 na shilingi 30,000.
 
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 34,557,864.41, maandalizi ya mchezo sh. 28,450,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 8,625,641.88.


Nyengine ni bonasi kwa timu ya Taifa Stars sh. 28,798,220.34, asilimia 15 ya uwanja sh. 18,917,141.01, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 25,222,854.67 na asilimia tano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), sh. 6,305,713.67. Asilimia 60 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), sh. 71,885,135.82 na Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,783,428.20 ambayo ni asilimia tano kutoka kwenye mgao wa TFF.
 
Katika hatua nyingine, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amewapongeza wachezaji wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi, mashabiki, mdhamini na serikali kwa kufanikisha ushindi wa juzi.
 
Tenga amesema ushindi huo umetokana na ushirikiano kutoka kwa wadau wote, na hasa wachezaji walioonesha kiwango kikubwa kulinganisha na mechi zilizopita ikiwemo kiwango cha kujituma uwanjani.
 
Amesema serikali ni mdau mkubwa wa mpira wa miguu katika miundombinu, usalama na idara zake mbalimbali ikiwemo Uhamiaji ambayo imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mechi hiyo.

1 comment:

  1. hivi kweli uchapishaji tiket 32,000 , zigharimu milioni 8 na zaidi? kila tkt inagharimu kiasi cha shs 250/= kweli? gazeti lenye kurasa kibao na mapicha bei yake ni shs 500/= hio na pamoja na kuuzwa kwa faida , tupo karne ya 21 lakini ulaji na wizi wa kificho ( sio spika wa bunge znz) bado unaendelea

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.