Habari za Punde

Ubakaji Washamiri Pemba


Na Rahma Juma,Saada Ali TSJ, Pemba
KESI 94 za ubakaji, udhalilishaji na unyanyasaji wa wanawake na watoto, zimeripotiwa katika kituo cha mkono kwa mkono kilichopo hospitali ya Chake Chake tokea kianze kazi Julai 2 mwaka jana hadi Febuari 27 mwaka huu.

Kesi hizo ni za ubakaji kesi (36), kulawiti (8), kutorosha (28), shambulio la aibu (5), shambulio la kuumiza mwili kesi 6 na kumpa mimba msichana asiyepata kuolewa kesi 11.

Akizungumza na waandishi wa habari hizi, Mratibu wa kituo hicho Pemba, Fatma Abdalla Ali, alisema kesi hizo zimekuwa zikiongezaka siku hadi siku hali inayowapa wasiwasi mkubwa.

Mratibu huyo alisema katika kesi hizo wilaya ya Chake Chake ndio inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya matukio hayo, ikiwa ni 76, wilaya ya Wete 9, Mkoani 7 na Micheweni ikiwa ndiyo yenye idadi ndogo kwa kuwa na kesi moja.

Aidha alifahamisha kuwa, wilaya ya Chake Chake imekuwa na idadi kubwa kutokana na wananchi wake kuwa na mwamko mkubwa wa kuripoti matukio hayo pale yanapotokea.

Hata hivyo alisema bado wilaya nyengine kama za Micheweni, Mkoani na Wete ambako wananchi wake wako mbali na kituo hicho, wana nafasi ya kuwasilisha kesi zao katika kituo hicho.

“Kila siku zikienda mbele, hali ya matuko haya kwa wilaya ya Chake Chake inazidi kuendelea, kwani tokea mwezi wa Januari hadi Febuari 27 mwaka huu, kesi 23 zimeripotiwa, hii ni takwimu kubwa sana,” alisema.

Aliwataka wananchi kuwa kitu kimoja katika kuripoti matukio hayo,pindi yanapotokea katika shehia zao.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili, alisema ni pamoja na usafiri wa kuyafuatilia matukio hayo, hususani vijijini, wakati wanapopewa taarifa na wananchi.

Hivyo ameziomba taasisi husika kuangalia uwezekano wa kukaa pamoja na serikali kuu ili kulitafutia ufumbuzi suala la usafiri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.