Na Mwanajuma Mmanga
Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamewalalamikia viongozi wa majimbo wa Mkoa kwa kushindwa kuwaunga mkono katika jitihada zao za kujiletea maendeleo.
Hayo yameelezwa na mmoja wa walemavu hao, Chagua Kundi Khamis, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi huko Matemwe wilaya ya Kaskazini Unguja.
Alisema viongozi wa majimbo wana wajibu mkubwa wa kutoa michango yao hususan kwa watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu ili kuondokana na utegemezi katika jamii, lakini jambo la kusahangaza viongozi hao hawawajibiki ipasavyo.
Aidha, amesema kufuatia kuweko kwa sera ya watu wenye ulemavu ambayo ilipitishwa kihalali na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini watu wengi wamekuwa hawaifanyii kazi sera hiyo, jambo ambalo linawakatisha tamaa watu wenye ulemavu.
Amesema kufuatia hali hiyo, ndio maana baadhi ya watu wenye ulemavu wanaonekana kuwa ombaomba kwa kukosa misingi madhubuti ya kujiajiri na kuonesha mambo yao.
Nae Sheha wa shehiya ya matemwe, Denge Khamisi Silima amekiri kuwepo kwa malalamiko hayo kwa viongozi wa jimbo kutotoa mashirikiano baina yao na wananchi katika kutatua kero zao za majimbo.
Denge alisema watu wenye mahitaji maalum wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo elimu kwa walemavu wasiosikia, miundombinu ya kisasa, ambayo kutawawezesha kuwasaidia kuona katika shughuli zao za kila siku.
Hata hivyo Sheha huyo amewataka viongozi hao kutoa mashirikiano ya karibu katika kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum ili kuwaondoshea matatizo yanayowakabili katika Shehia yao.
Pia amewaomba viongozi hao wa majimbo kusaidia kuwasomesha walemavu wasiosikia na kupewa taaluma ya kusomesha, itayowasaidia usikivu na uelewa wa kutosha.

No comments:
Post a Comment