Habari za Punde

Abdulhalim Humud afuzu majaribio Jomo Cosmos

Na Elizabeth John
 
KIUNGO wa Azam FC, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ amefuzu kucheza soka la kulipwa katika timu ya Jomo Cosmos FC ya Daraja la Kwanza nchini Afrika Kusini.
Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Mtibwa Sugar ya Morogoro na Simba, amekuwa akikosa namba ya kudumu katika kikosi cha Azam kwa zaidi ya misimu miwili, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kuwa majeruhi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Msaidizi wa Azam FC, Jemedari Said, alisema Humud amefanikiwa kufuzu majaribio katika timu hiyo na kilichobaki ni pande hizo kujadiliana ada ya uhamisho.
“Kwa ufupi Humud amefuzu kila kitu huko Afrika Kusini na muda wowote atarudi nchini kuja kumalizia taratibu zingine za uhamisho, na tuna imani ataiwakilisha timu yetu vizuri, pamoja na taifa lote kwa ujumla,” alisema Jemedari.

Akimzungumzia Humud, alisema ni mchezaji mzuri na mwenye kiwango cha juu, lakini amekuwa akipata wakati mgumu kupata namba mara kwa mara, kutokana na ushindani mkali uliopo hivi sasa katika timu yao.
Alisema kwa mujibu wa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’, Jomo Sono, ambaye pia ndiye mmiliki wa Cosmos walitoa nafasi hiyo kwa Humud kutokana na kuwa na uhusiano mzuri na Azam na pia kuridhishwa na kiwango cha kiungo huyo.
 
Chanzo - Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.