Habari za Punde

Dk. Shein aihakikishia amani Uingereza


Na Said Ameir, Ikulu
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amemhakikishia Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose kuwa Zanzibar itaendelea kuwa salama na tulivu kwa sababu serikali na wananchi wake wameamua kuendeleza utamaduni wao wa kuishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana.

Dk. Shein alimueleza balozi huyo ambaye alifika Ikulu kujitambulisha kuwa viongozi wa serikali iliyo chini ya mfumo wa umoja wa kitaifa wameonesha mfano wa utamaduni huo kwa kufanya kazi kwa pamoja pasi na kuonesha tofauti zao za vyama wala itikadi ya kisiasa.

“Tumepiga hatua kubwa kudumisha amani na utulivu kwa sisi viongozi wa serikali kuonesha mfano kwa kushikamana na kufanyakazi kwa pamoja bila ya kuonesha tumetoka vyama tofauti vya siasa na hivyo hivyo kwa wananchi tunaowaongoza,” alisema Dk. Shein.

Rais alisema serikali imekuwa ikifanya vizuri katika kuwatumikia wananchi na imefurahishwa na namna washirika wa maendeleo ikiwemo Uingereza inavyoziunga mkono jitihada za serikali za kuinua uchumi na kupambana na umasikini.

Aliishukuru Serikali na wananchi wa Uingereza kwa misaada yake katika sekta mbalimbali za maendeleo na kueleza matumanini yake kuwa pande mbili hizo zitaangalia maeneo mapya ya ushirikiano ili kuimarisha uhusiano uliodumu kwa miaka mingi kati ya Uingereza na Tanzania.

Alitumia fursa hiyo kumtumia tena salamu za pole Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na wananchi wa nchi hiyo kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Margret Thatcher aliyefariki wiki iliyopita.

Kwa upande wake balozi Melrose amemweleza Rais kuwa amefurahi kupewa heshima kuitumikia nchi yake nchini Tanzania nchi ambayo imekuwa na uhusiano thabiti na wa miaka mingi.

Alisema Uingereza itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kuinua hali ya maisha ya wananchi wake na kuongeza kuwa wakati wa kipindi cha utumishi wake nchini atahakikisha uhusiano kati ya serikali na wananchi wa Uingereza na Zanzibar unazidi kuimarika.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.