Habari za Punde

Nchemba asisitiza kuwa na CD za hujma

Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba amedai kuna ukanda mzima wa CD wa mpango hujuma na hakuna haja kwa baadhi ya Wabunge kuwa na wasiwasi juu ya madai hayo kwani wakati ukifika ataweka wazi.

Nchemba aliyasema hayo jana wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, inayoendelea kuchangiwa, matangazo ambayo yanarushwa moja kwa moja na TBC1.

Alisema anashangaa kuona baadhi ya Wabunge kuja ndani ya bunge hilo na rundo la namba za simu huku wakitaja maafisa wakubwa katika Idara ya Usalama wa Taifa wakati wakijua ukanda wa maandalizi ya hujuma upo na ikifika wakati ataweka hadharani.

Matamshi ya Nchemba yamekuja baada ya kutokea mvutano mkali ndani ya bunge baada ya upinzani kudaiwa kuingiza vipengele vinavyojadili mwenendo wa Idara ya Usalama wa Taifa na baadhi ya masuala yaliyopo mahakamani katika hotuba yao.

Mbunge wa Kigoma mjini, Peter Serukamba alisema ukurasa wa kwanza hadi wa nne wa hotuba hiyo, hazikutakiwa kusomwa katika bunge hilo kwa kuwa zilikuwa zikizungumzia kesi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare iliyopo mahakamani.

Kauli hiyo ilisababisha Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), kusimama na kutoa taarifa akisema Mbunge huyo hakuwa na uhalali wa kupinga hotuba ya upinzani kwa kuwa anacholalamikia kilikuwa hakijasomwa.

Pia, alisema matukio ya kutekwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka na Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, hayakuwa mahakamani.

Dakika kumi kabla ya muda wa kawaida wa Bunge, Naibu Spika, Jobu Ndugai, alilazimika kukatisha hotuba hiyo iliyokuwa ikisomwa na msemaji wa kambi hiyo, kuhusu Wizara ya Katiba na Sheria, na kuliahirisha Bunge hilo kabla ya muda wake wa kawaida lakini wakati wa jioni kulijitokeza vuta nikuvute iliyosababisha Wabunge sita wa Chademna kutolewa nje.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda, amesema mabadiliko yanayofanywa ndani ya Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) hayana nia ya kuharibu uchaguzi mkuu ujao ila serikali inaweka mazingira bora kama nchi nyingine zinavyofanya.

Aliyasema jana wakati akijibu maswala ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge.

Akijibu hilo suala la kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, Pinda, alisema utaratibu wa zamani wa uandikishaji wa wapiga kura umekuwa ukilalamikiwa mara kwa mara wa kuhesabu kura kwa kutumia vidole lakini utaratibu mpya unaweza kuondoa malalamiko.

Alisema nchini Kenya ingawa waliamua kufanya kazi kwa kutumia mfumo wa kisasa lakini walijikuta wakirudi katika utaratibu wa kuhesabu kura kwa mikono.

Alisema suala la kuwahusisha wadau, alisema hilo linaweza lisifanyike kwa vile mfumo huo uko kitaalamu zaidi na unaweza kufikia lengo ambalo serikali inakusudia kulifanya.

Akizungiumzia juu ya serikali kudaiwa kumzuiya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamadi kwenda Mtwara, alisema suala hilo lilijitokeza kutokana na hali ya usalama katika mkoa huo wakati huo, akisema usalama haukuwa nzuri.

Alisema katika kipindi hicho Maalim Seif, hakuwa na dhamira ya kufanya shughuli za maendeleo bali aliomba kwenda huko kwa mambo ya kisiasa na serikali haikuwa na nia mbaya ya kumzuiya kiongozi huyo.

Aidha alisema serikali haiwezi kupiga marufuku uendeshaji wa pikipiki aina ya boda boda kwani zimesaidia vijana wengi kujiajiri na kupunguza tatizo la usafiri nchini hasa vijijini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.