Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na waislamu mbali mbali alipofika Mwera kwa ajili ya ufunguzi wa Masjid Maulana.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akifungua pazia kuashiria ufunguzi wa Masjid Maulana ulioko Mwera.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi funguo za msikiti kwa Mzee wa “Masjid Maulana” ulioko Mwera, Sheikh Soud, katika hafla ya ufunguzi wa msikiti huo. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Hassan Hamad (OMKR)
Viongozi wa misikiti wametakiwa kutunza nidhamu katika nyumba hizo za ibada, na kuachana na tabia ya kugombaniana uongozi, ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Al-hajj Maalim Seif Sharif Hamad katika hafla ya ufunguzi wa “Masjid Maulana” ulioko Mwera, katika Wilaya ya Magharibi Unguja.
Amesema misikiti ni nyumba za ibada, hivyo hakuna sababu kwa waislamu kugombania misikiti, na badala yake viongozi watakaochaguliwa wawajibike kutunza nidhamu na kuendeleza harakati za kiibada ikiwa ni pamoja na kuendeleza darsa na mijadala ya kuuendeleza Uislamu.
Maalim Seif amewataka waumini wa msikiti huo kushirikiana na kusaidiana katika mambo mbali mbali ya kijamii, sambamba na kuchangia harakati za misikiti kwa kuhakikisha kuwa wanasaidia kutatua kasoro zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Ngwali, amesema waislamu wana wajibu wa kuitunza na kuihifadhi misikiti, ili iweze kuwa katika hali nzuri na usafi wakati wote.
Amesisitiza haja kwa waislamu kuitumia misikiti kwa shughuli za ibada na elimu, na kuwataka viongozi kuwa mifano bora katika jamii juu ya kuendeleza maadili ya kiislamu na ibada.
Hassan Hamad (OMKR)
No comments:
Post a Comment