Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na baadhi ya Familia ya Bi Kidude wakati alipofika kutoa mkono wa pole kwa ndugu na jamaa wa msanii huyo.
Kushotoya Balozi ni Nd. Haji Ramadhani Suwed na kulia ni Bwana Abdulrahman Saleh.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika dua ya pamoja na kutakia malazi mema Gwiji la sanaa Zanzibar Bi Ftma Binti Baraka { Bi Kidude } hapo nyumbani kwake Rahaelo nyuma ya Studio ya ZBC Redio.
Kulia ya Balozi Ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Nd. Borafia Mtumwa na Kushoto yake ni Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo Mh. Nassor Al – Jazira.
Picha n Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kugharamia mazishi ya Gwigi la Sanaa ndani ya ukanda wa Afrika ya Mashariki na mipaka yake Anti Fatma Binti Baraka { Maarufu Bi Kidule } aliyefariki dunia juzi mchana baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mchango wake katika kuitangaza sanaa ya Zanzibar nje ya mipaka ya Tanzania hasa kwenye fani ya muziki wa Taarabu asilia na ile ngoma maarufu ya Unyago inayotumika katika sherehe za harusi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiifariji familia ya Marehemu Bi Kidude wakati wa matayarisho ya mazishi yake hapo Mtaani kwake Rahaleo nyuma ya Kituo cha ZBZ Redio Rahaleo Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akitoa ubani wa shilingi Milioni 2,000,000/- kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa familia ya marehemu alisema jamii na waswahili wote katika mwambao wa Afrika Mashariki wanafahamu mchango mkubwa wa Msanii Bi Kidude katika fani ya muziki wa taarabu.
Alisema Zanzibar imepata sifa kubwa katika Nyanja za Kimataifa kutokana na mchango wa wasanii kwa kueneza sanaa ya Taarabu iliyotoa fursa kwa baadhi ya watalii na wataalamu kuvitembelea Visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameitaka Familia ya Msanii Bi Kidude kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba na kuwaeleza kwamba msiba huo sio wao peke yao.
“ Kwa kweli sisi sote tunampenda sana Bi Fatma Binti Baraka { Bi Kidude }. Lakini tuelewe kwamba Mwenyezi muungu anampenda zaidi na ndio maana akamuhitaji Bi Kidude “. Alinasihi Balozi Seif.
Naye Mmoja wa wana Familia hiyo Bwana Haji Ramadhan Suwed Buda kwa niaba ya Familia ya Marehemu Bi Kidude ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake wa kuungana nao katika msiba huo.
Bwana Haji alisema hatua hiyo ya Serikali imeleta faraja kwao na kupunguza machungu ya msiba huo.
Msanii Gwiji wa sanaa ya Taarab asilia na ngoma ya Unyago Marehemu Bi Kidude aliyekadiriwa kufikia umri wa zaidi ya miaka 98 hakuwahi kuolewa wala kupata Mtoto.
Mwenyezi Muungu ailaze roho ya marehemu Bi Kidude mahali pema peponi amin.
No comments:
Post a Comment