Habari za Punde

Zanzibar yashauriwa kuyatumia makampuni ya maji kujinasua na uhaba wa huduma ya maji

  Mwakilishi wa Makampuni ya Ulinzi na Maji ya Botjheng Water na Megatron yenye Makao Mkuu yake Nchini Afrika Kusini Bwana Dean Hirani akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 Bwana Dean Hirani anayesimamia pia biashara za Kimataifa, Masoko, Ushauri na Fedha katika Mataifa ya Bara la Afrika .
Picha na Hassan Issa wa - OMPR – ZNZ .
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR

Zanzibar imeshauriwa kuyatumia Makampuni yanayojishughulisha na masuala ya maji na ulinzi wa visiwa katika harakati zake za kujinasua na uhaba wa huduma za maji pamoja na uhakika wa ulinzi wa maeneo yake.
Ushauri huo umetolewa na Mwakilishi wa Makampuni ya Ulinzi na Maji ya Botjheng Water na Megatron yenye Makao Mkuu yake Nchini Afrika Kusini Bwana Dean Hirani wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Dean Hirani anayesimamia biashara za Kimataifa, Masoko, Ushauri na Fedha katika Mataifa ya Bara la Afrika alisema Makampuni hayo yenye Utaalamu wa Kimataifa tayari yamekuwa yakitoa huduma katika Mataifa Kadhaa Barani Afrika.

Alisema Wataalamu wa Kampuni ya Maji wamefikia hatua ya kuyabadilisha maji ya bahari kutumika katika matumizi ya kawaida ili kupunguza utegemezi wa maji yanayopatikana chini ya ardhi.
Bwana Dean alifahamisha kwamba utaratibu unaotumiwa na wataalamu wa kuchimba maji chini ya ardhi kwa kiasi Fulani unachangia mmong’oko wa ardhi na hatimae kuhatarisha uchafuzi wa mazingira.
Kuhusu suala la ulinzi wa Visiwa Bwana Dean alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Kampuni ya Megatron imeanzisha mfumo wa utoaji mafunzo kwa askari pamoja na vikundi vya ulinzi ambao unaenda sambamba na utoaji wa Boti za doria zinazotumiwa na walinzi hao.
Alieleza kuwa vikundi vya ulinzi hupatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo katika vituo vya Afrika Kusini na Spain ambapo nchi kadhaa za bara la Afrika kama Nigeria,Angola, Cameroun na Tanzania Bara zimeshatumia fursa hiyo kwa kupeleka vijana wao.
Msimamizi huyo wa biashara za Kimataifa, Masoko, Ushauri na Fedha katika Mataifa ya Bara la Afrika wa Makampuni ya Botjheng Watern na Megatron Bwana Dean Hiran alisema Makampuni hayo yako yatari kutoa nafasi ya upendeleo wa kuisaidia Zanzibar katika maeneo ambayo yatapendekezwa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inahitaji huduma zote zinazotolewa na Makampuni hayo kutokana na mazingira yake hasa lile suala la ulinzi wa Visiwa.
Balozi Seif alisema yapo matatizo yanayofanywa na wavuvi wa Kimataifa kwa kujichukulia rasilmali za Zanzibar zilizomo baharini bila ya wasi wasi kutokana na uwezo wao mkubwa wa vyombo vya uvuvi wanavyovimiliki.
Alisema uwepo wa mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni hiyo ya Megatron unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo kwa vile ulinzi wa doria unakuwa wa uhakika kwa kukabiliana na wahalifu hao.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.