Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kufuta hati zote ilizozitowa kwa ajili ya matumizi ya Ardhi ambazo wamepewa baadhi ya watu kwa shughuli za ujenzi au uwekezaji ambapo watu hao wahajazifanyia lolote ardhi hizo kwa kipindi kirefu sasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa Kiwanda kipya cha Maji ya Kunywa { Drinking Mineral Water Process Boiling Plant } kinachomilikiwa na Kampuni ya Safari hafla iliyofanyika katika maeneo huru ya Viwanda yaliyopo Amani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema kumekuwa na mrundikano wa maeneo kadhaa ya ardhi yalizozunguushwa ukuta ambayo Serikali tayari imeshayagundua na kumuagiza Waziri anayehusika na Ardhi kuwafutia mara moja hati ya usajili wa matumizi wahusika hao.
Alisema tabia hiyo mbaya kwa kiasi Fulani imekuwa ikichangia kuviza maendeleo ya uwekezaji hapa Nchini na kuwakatisha Tamaa watu na makampuni yenye nia ya kutaka kuwekeza Vitega uchumi vyao hapa Nchini.
“ Mimi na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar tumeshakubaliana kukabiliana na tatizo hili sugu, kwani tayari Waziri anayehusika na masuala ya Ardhi ameshaagizwa kufuta hati ya matumizi kwa mtu aliyeshindwa kuitumia ardhi hiyo “. Alitahadharisha Balozi Seif.
“ Wapo watu waliojilimbikizia maeneo makubwa ya ardhi kwa tamaa ya kuyauza baadaye kitendo ambacho ni kinyume na sheria na taratibu za Serikali. Wanajiuzia ardhi na kusahau kwamba ardhi yote ni mali ya Serikali na ndio yenye uwezo na mamlaka ya ardhi hiyo itumike kwa shughuli gani “. Alionya Balozi Seif.
Akizungumzia suala la Uwekezaji Balozi Seif alisema Wawekezaji katika Sekta ya Viwanda hapa Nchini wana wajibu wa kuhakikisha bidhaa wanazozizalisha zinakuwa katika kiwango kinachokubalika Kitaalamu ili kukabiliana vyema na soko la Dunia sambamba na kuitangaza Zanzibar Kimataifa.
Alisema wanaofanikiwa kwenye uzalishaji huo wa bidhaa katika mauzo ya Kimataifa ni wale wawekezaji wanaojikita zaidi katika kuzalisha bidhaa bora zaidi na kuuza kwa bei nafuu.
Balozi Seif alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kujenga umaarufu wa kusafirisha bidhaa mbali mbali zinazozalishwa kwenye viwanda vya hapa Nchini.
Alisema hatua hii ni miongoni mwa azma ya Serikali ya kuimarisha Uchumi kwa kuwa na viwanda vingi Nchini vitakavyosaidia kukuza uchumi na hatimae kupunguza zaidi tatizo la ajira linalowakabili Vijana walio wengi.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Sekta ya Viwanda bado inaendelea kutoa ajira hafifu ikilinganishwa na Sekta nyengine. Hivyo jitihada za ziada zinahitajika kuchukuliwa katika kukaribisha wawekezaji kwa upande wa Sekta hiyo ya Viwanda.
Alisema kwa mujibu wa sera ya uwekezaji ya Zanzibar, Sekta ya uzalishaji bidhaa viwandani imepewa kipaumbele kutokana na kuwa na tija kubwa kiuchumi na Kijamii kwa vile ina wigo mkubwa wa shughuli za kibiashara ambapo watu wengi wanaweza kufaidika nazo.
“ Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar imeazimia kukuza uchumi na kupunguza umaskini, kama ilivyoeleza katika Mpango wake unaojuilikana kama Mkuza ambao umetokana na Dira ya Maendeleo ya 2020 “. Alifafanua Balozi Seif.
Aliupongeza Uongozi wa Kampuni ya Safari kwa uamuzi wake wa kuanzisha Mradi huu mpya wa kiwanda cha maji ya kunywa unaotarajiwa kutoa ajira za wafanyakazi wazalendo 40 ikiwa ni mafanikio makubwa ya kupunguza wimbi la Vijana wasiokuwa na ajira.
Alifahamisha kwamba Zanzibar imekuwa maarufu kibiashara kwa kuagiza bidhaa mbali mbali nchi za nje ikiwemo pia maji, mfumo ambao kwa wakati huu unafaa kupunguzwa.
Alisema Utegemezi huu wa kuagiza kila kitu kutoka nje ya Nchi unaweza kudhoofisha mfumo wa fedha za kigeni zilizopo hapa Nchini na kupelekwa nje ya Zanzibarkwa ajili ya biashara hizo.
Akizungumzia Bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vya hapa Nchini Balozi Seif alitoa wito kwa wenye viwanda hivyo kuweka bei pungufu kwa bidhaa zenye kasoro endapo kasoro hizo hazitoleta madhara kwa watumiaji utaratibu ambao hufuatwa na nchi nyingi zinazozalisha bidhaa za viwandani.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona bidhaa zenye kasoro bado huendelea kuuzwa kwa bei ile ile inayolingana na bidhaa isiyo na kasoro. Hivyo ipo haja ya kufunguliwa maduka maalum kwa ajili ya uuzwaji wa bidhaa zenye kasoro zikiwa na bei pungufu.
Kuhusu mazingira Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wawekezaji kufuata sheria ya mazingira na Serikali itahakikisha Viwanda vinavyojengwa Nchini vinafuata na kuzingatia taratibu zote za kutunza mazingira.
Balozi Seif alionya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitomuonea muhali mwekezaji ye yote atakayejaribu kwenda kinyume na masharti yaliyowekwa ya utunzaji wa mazingira.
Mapema Mkurugenzi na Mmiliki wa Kampuni ya Safari inayomiliki Kiwanda hicho cha Maji ya kunywa Bibi Mala Kalwan alisema ukarimu wa Wazanzibari na mazingira mazuri yaliyopo Zanzibar ndio chachu iliyoipa Kampuni hiyo kupata hamasa ya kuwekeza vitega uchumi vya hapa Zanzibar.
Bibi Mala Kalwan ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Taasisi ya uwekezaji Vitega uchumi Zanzibar { ZIPA } kwa mashirikiano mazuri yaliyopelekea kufanikisha uwekezaji huo wa Kiwanda cha Maji.
“ Hatuna budi kuipongeza ZIPA kwa juhudi zake za kutuunga mkono kwa asilimia kubwa baada ya kukamilisha sheria na taratibu za Uwekezaji “. Alisisitiza Bibi Mala Kalwan.
Alisema Kampuni yake katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha Uchumi wake ina mpango wa kuongeza mradi mwengine wa kiwanda cha Juisi na kuifanya Kampuni hiyo kuwa na Viwanda vinne hapa Zanzibar vikitambuliwa na viwanda vya kanda za kurikodia sauti kiwanda cha vyombo vya nyumbani na Maji ya Kunywa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Nd. Salum Khamis alisema ipo miradi 519 iliyopitishwa na ZIPA kati ya Miradi 788 iliyopokelewa hadi mwezi Machi mwaka huu wakati ambapo miradi 269 imefutwa miongoni mwa hiyo.
Nd. Salum alisema miradi ya Viwanda pekee hadi sasa imefikia 47 na kusaidia kutoa ajira kwa wafanyakazi 79 ambao kati ya hao wafanyakazi 69 ni Wazalendo.
Mkurugenzi Mtendahi huyo wa ZIPA alisisitiza kwamba sera ya uwekezaji Zanzibar inalenga kuunga mkono wawekezaji wazalendo ambao wana fursa zaidi ya kuchangia pato la Taifa.
Mradi huo wa Kiwanda cha Maji ya kunywa cha Super Shine umegharimu jumla ya Dolla za Kimarekani Milioni Moja na Laki mbili.
Hongara kwa kauli tunasubiri vitendo tuone wananchi watoshwa na viongozi wa poraji
ReplyDelete