Habari za Punde

Mama mbaroni kwa kumfukia mtoto akiwa hai

Na Rose Chapewa, Morogoro
JESHI la polisi mkoani Morogoro linamshilikia Joyce Kodi (24) mkazi wa kijiji cha Ngweranga, kilichopo Malinyi wilayani Ulanga kwa tuhuma za kujifungua mtoto wa kike kisha kumfukia nyuma ya nyumba yake akiwa hai na kusababisha kifo chake.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, John Laswai alisema mwanamke huyo alitenda kosa hilo Mei 7 mwaka huu majira ya saa 1: 30 asubuhi nyumbani kwake katika kijiji cha Ngweranga.
Alisema alijifungua mtoto huyo akiwa hai, na katika hali isiyokuwa ya kawaida aliamua kuchimba shimo nyuma ya nyumba yake kisha kumfukia na kusababisha kifo chake.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi, pamoja na madaktari kumfanyia uchunguzi wa kiakili mwanamke huyo, na kwamba atafikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Alisema katika tukio jingine mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aliyefahamika kwa jina la Issa Bakari mkaazi wa Mafisa manispaa ya Morogoro alikufa baada ya kuzama kwenye mto Ngerengere.
Kamanda Laswai alisema tukio hilo lilitokea Mei 8 mwaka huu saa 3:45 asubuhi, kwenye mto huo eneo la Mafisa na kwamba uchunguzi unaendelea zaidi.
Wakati huo huo mpiga deba aliyefahamika kwa jina la Nelson Haule (31) mkazi wa Mtawala mjini hapa alifariki akiwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro akipatiwa matibabu baada ya kulazwa baada ya kuanguka ghafla.
Alisema mpiga debe huyo alianguka ghafla katika eneo la Hamjuki, ambapo alikimbizwa hospitali na Mei 5 majira saa 5 usiku alifariki dunia, uchunguzi unaendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.