Habari za Punde

Balozi Seif ataka mripuko Arusha usihusishwe na dini, siasa


Othman Khamis na Mwantanga Ame, Arusha
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewaasa watanzania kuacha dhana ya kulihusisha tukio la mripuko unaodhaniwa kuwa ni bomu uliotokea katika Kanisa katoliki Wilayani Arumeru Mkaoni Arusha lisihushishwe na masuala ya kidini wala kisiasa.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo alipofanya ziara fupi ya kuangalia majeruhi wa mripuko huo waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha pamoja na kuwapa pole Viongozi pamoja na waumini wa Kanisa lililopata maafa hayo.

Balozi Seif alisema tukio hilo ambalo lina dalili zote za Kigaidi limeshitua Taifa na kuwakera wananchi wote Tanzania Bara na Zanzibar na linafaa kulaaniwa na wapenda amani wote popote walipo.

Alifahamisha kwamba hiyo ni fitna inayojengwa katika kuleta chuki baina ya Serikali na wananchi hasa waumini. Hivyo aliwanasihi Watanzania kuendelea kutulia na wala hakuna haja ya kuanza kutuhumiana ndani ya kipindi hichi kigumu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea haja yake kufuatia vyombo vya ulinzi kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wahusika wa mripuko huo wapatao 10 hadi hivi sasa ambao kati yao wanne ni raia wa Saudi Arabia na mmoja raia wa Kenya.

Balozi Seif aliwahakikishia wananchi wote pamoja na waumini walioathirika na tukio hilo kwamba Serikali itahakikisha inawashikilia wale wote waliohusika na njama hizo na kuwachukulia hatua za kisheria kutokana na udhalimu wao huo.

“ Tungeliomba jambo hili baya lisitokezee tena katika nchi yetu kwani linaonesha kuleta fitna kati ya Serikali na wananchi wake “ alisisitiza Balozi Seif.

Akizungumzia suala la kidini, Balozi Seif alisema Serikali zote mbili zimetoa uhuru wa kuabudu ambao umo ndani ya katiba na kamwe haitavumilia kuona uhuru huo unaingiliwa na watu wachache.

Alisema matukio ya hujuma ndani ya majengo ya ibada yamekuwa yakiwapa hofu na wakati mgumu waumini kuendelea na ibada zao za kila siku.

“Hofu hii iliyojengeka miongoni mwa waumini kutokana na hujuma wanazofanyiwa inawapa wakati mgumu wa kuabudu waumini hao “, alifafanua Balozi Seif.

Akitoa shukrani kwa niaba yake na waumini wenzake Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Askofu Josephat Leburu alisema waumini wa jimbo hilo wamepata fafaja kubwa kufuatia ujio wa viongozi mbali mbali wa Kitaifa waliofika kuwapa pole.

Askofu Josephat alisema moyo huu ulioonyeshwa na Viongozi wa Kitaifa umetoa sura sahihi iliyoonesha ushirikiano wa karibu yao yao na wananchi wanaowaongoza.

Hata hivyo Viongozi hao wa Kidini waliiomba Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi kuendelea kutoa taarifa kadri hatua zinavyochukuliwa za kukabiliana na tukio hilo waliloliita la kigaidi.

Walisema hatua hiyo itasaidia sana kupunguza joto la waumini wao ambalo wakati mwengine hufikia maamuzi ya kutaka kuchukua hatua mikononi mwao wanapokabiliwa na matukio ya hujuma dhidi yao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Nyerembe Munasa Sabi, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya changamoto za waumini hao alisema Serikali kuu kupitia, Mkoa na Wilaya hiyo inaendelea na juhudi za kuwasaka wale wote waliohusika la mripuko huo.

Nyerembe alifahamisha kwamba hadi sasa watuhumiwa kumi wameshatiwa mbaroni kwa msaada wa wananchi wema ambapo kati yao wanne ni raia wa Saudi Arabia na mmoja Raia wa Kenya.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru alieleza kwamba tukio hilo la mripuko ni ishara ya ugaidi unaojenga chuki ambao umeandaliwa katika mazingira ya kitaalamu zaidi.

Aliwanasihi viongozi na waumini wa Kikristo Mkoani humo kuendelea kuwa wastahamilivu wakati Serikali kuu inajitahidi kujenga mazingira yatakayosaidia kuepusha mgawanyiko miongoni mwa wananchi.

Nyerembe pia alikemea tabia ya baadhi ya wanasiasa kuanza propaganda ya kulinasibisha tukio hilo kuwa na uhusiano na Chama cha siasa.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru alieleza kuwa hadi sasa mripuko huo ulisababisha vifo vya watu watatu, na wengine 66 kujeruhiwa ambapo mpaka muda huu watu 24 wamesharuhusiwa kurejea nyumbani na wengine 34 wanaendelea kupata huduma katika hospitali ya Mkoa ya Arusha.





2 comments:

  1. Huyu bwana ni mtu wa ajabu ingekuwa mripuko ule umetoke huku Zanzibar engesema ni siasa na dini bila ya vyombo husika kutoa kauli,haijambo kauli alio itoa huko Arusha ni nzuri hakufanya vituvyake

    ReplyDelete
  2. Damu Nzito kuliko maji bwanaa.. Hataki Nchi yake ya Tanganyika iingie kwenye matatizo.. Lakini zanzibar ikiingia kwenye matatizo wanaofaidika ni Akina Seifu Mweusi.. Mshenzi Mkubwa huyo.., Usowake na roho yake haina tofauti...

    Yle mkewe amekwenda Pemba kutoa pesa za Mkopo, kwa vikundi vya Ushirika. Wakati Pesa hiyo ni ile anayopokea kutoka Hisa za Hoteli zote za Unguja na Pemba... Bila yakuzilipia Kodi...

    Kuwemo huyu ndani ya Serikali ya Umoja ni kama mtu kutiwa Virusi vya Ukimwi... Ni yeye ndie ameiharibu haiba ya Serikali ya Umoja.. Mshenzi mkubwa laghana tullahi.. Atwambie ziko wapi pesa za Michango ya kuzama kwa Meli?

    au ndio hizo wanazopita wakigawa..

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.