Habari za Punde

Pinda:Tusishabikie maafa ya wenzetu

Na Mwandishi wetu, Arusha
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewaonya baadhi ya watu wanaofanya ushabiki wa kisiasa kwenye tukio la mripuko wa Arusha na kuwataka wasitumie tukio hilo kujipatia umaarufu na badala yake watumie fursa hiyo kuwafariji walioathirika na kuwa watulivu hadi suala hilo lifikie hatma yake.

Alisema tukio hilo ni kubwa, na kitendo hicho ni kibaya kinachostahili kulaaniwa vikali kwa hiyo haifai watu wachahe kujipatia umaarufu kupitia tukio hilo.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwatembelea ili kuwajulia hali majeruhi waliolazwa hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na hali ya utulivu wa wananchi wa Arusha na hasa walio karibu na kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, kufuatia mripuko wa mabomu uliotokea Jumapili iliyopita, Mei 5, mwaka huu.

Alisema ameguswa pia na hali ya matibabu inayotolewa kwa majeruhi.

Waziri Mkuu alikatisha shughuli za bunge juzi mchana na kuelekea Arusha.

Mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA, Waziri Mkuu alikwenda moja kwa moja Parokia ya Olasiti ili kujionea hali halisi na kuwapa pole wamunini wa kanisa hilo.

Baadaye alikwenda kumjulia hali Askofu wa jimbo kuu la Arusha, Mhashamu Josephat Lebulu pamoja na Balozi wa Vatican, Mhashamu Askofu Fransisko Padilla ambako alifanya nao mazungumzo na kuwahakikishia viongozi hao kwamba serikali itafanya kila iwezalo hadi iwabane wahusika.

Akiwa hospitali ya Mount Meru, Pinda alimweleza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti kuwa asisite kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo endapo hali ya majeruhi itabadilika na watahitaji matibabu zaidi.

Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 23.3 ambavyo ni dawa na vifaa tiba kwa uongozi wa hospitali hiyo ambavyo vilitolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) chini ya uhamasishaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kukabidhi misaada hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema TANAPA ilitoa mablanketi 50 kwa hospitali hiyo na kwamba wafanyabiashara wa sekta ya utalii wa mjini Arusha wamejipanga kutoa msaada zaidi ili kuisaidia hospitali hiyo kumudu kuwahudumia majeruhi .

Hadi sasa, watu watatu wamepoteza maisha kutokana na mripuko huo ambapo watu wanane wamekamatwa na kuhojiwa na polisi.

Kati yao, wanne ni raia wa Saudi Arabia na waliobakia ni wakazi wa Arusha.

Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tulio hilo.

Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema wagonjwa watatu wana hali mbaya ambapo mgonjwa mmoja yuko Muhimbili na wawili wako Mount Meru.

“Watu 66 waliathirika na mripuko huo, watatu wamefariki na kati ya wagonjwa 63 waliobakia, wagonjwa 24 wamesharuhusiwa kurudi nyumbani, waliobakia wanaendelea kupatiwa matibabu,” alisema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amelithibitisha Bunge kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kitu kilichotumika kushambulia kanisa lilikuwa bomu la kutupwa kwa mkono.

Hata hivyo, alisema uchunguzi kuhusiana na tukio hilo bado unaendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.