Habari za Punde

Maalim Seif ahimiza Watanzania kuepuka kubaguana

   Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Matha Umbula, wakati alipowasili uwanja wa ndege wa Dodoma kwa ziara ya siku mbili katika mikoa ya Manyara na Singida
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akipokelewa na viongozi wa Mikoa ya Dodoma, Manyara, Singida pamoja na baadhi ya Wabunge wa CUF, wakati alipowasili uwanja wa ndege wa Dodoma kwa ziara ya siku mbili katika mikoa ya Manyara na Singida.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na vikosi vya ulinzi na usalama, wakati alipowasili uwanja wa ndege wa Dodoma kwa ziara ya siku mbili katika mikoa ya Manyara na Singida
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiweka jiwe la msingi katika nyumba ya watumishi wa Zahanati ya Kiperesa, Wilaya ya Kiteto.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wananchi wa Matui, Wilaya ya Kiteto.
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara Martha Umbula, akitoa salamu za Mkoa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, alipotembelea kijiji cha Kiperesa. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Hassan Hamad, OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewahimiza watanzania kuendeleza utamaduni wa kuishi pamoja na kushirikiana bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
 
Amesema utamaduni huo ndio msingi wa maendeleo ya nchi na wananchi wake, na kinyume chake ni kukaribisha migogoro na mifarakano isiyokuwa ya lazima.
 
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF ameeleza hayo kwa nyakati tofauti wakati akiwa katika ziara ya kutembelea vijiji mbali mbali vya Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara.
 
Katika ziara hiyo Maalim Seif alipata fursa ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo na baadaye kufungua msikiti wa Arahaman katika kijiji cha Chekanao, kutembelea kijiji cha Matui na kuweka mawe ya msingi katika nyumba ya watumishi wa Zahanati ya Kiperesa na ofisi ya kijiji hicho.

Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo Maalim Seif amewataka kuiga mfano wa Zanzibar katika kuendeleza amani ya nchi, na kwamba Zanzibar sasa inapiga hatua kubwa za maendeleo tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
 
Amesema chini ya Serikali hiyo wafanyakazi wameongezewa mishahara kwa asilimia 25, sambamba na kuongeza bei ya karafuu na kuwawezesha wakulima wa zao hilo kupata asilimia 80 ya soko la dunia.
 
Kuhusu sera za CUF Maalim Seif amesema ni pamoja kujenga uchumi ambao utawanufaisha watanzania wote bila ya kujali mahali walipo au wanapotokea.
 
Amesema iwapo CUF kitapata mamlaka ya kuongoza nchi, kitaweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa kila mtanzania ananufaika na mapato yatokanayo na rasilimali za nchi, na kwamba hatua hiyo pia itasaidia wananchi kuzilinda rasilimali za nchi yao.
 
Katika ziara hiyo Makamu wa Kwanza wa Rais amechangia zaidi ya shilingi milioni moja kwa ajili ya maendeleo ya msikiti na kijiji cha Kiperesa.
 
Mapema akisoma ripoti ya utekelezaji wa kata ya Uroboti Wilaya ya Kiteto, afisa mtendaji wa kata hiyo bibi Zainab Mahiza amesema kata yao inakabiliwa na matatizo kadhaa yakiwemo upungufu wa madarasa na vikalio, vitendea kazi na matumizi mabaya ya ardhi.
 
Maalim Seif ambaye alipokelewa rasmi katika uwanja wa ndege wa Dodoma, amemaliza ziara ya siku moja katika Wilaya ya Kiteto na atamalizia ziara yake katika Mkoa wa Singida.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.