Habari za Punde

Mtuhumiwa wizi wa n'gombe ayakana maelezo yake

Na Asha Salim, Pemba

KIJANA  Haroub Muhamed Hamad (22) mkaazi wa Ole Kianga apatiwa onyo la mwisho katika Mahkama ya wilaya Chake chake kwa kosa la kukataa kufahamu utaratibu wa mahkama chini ya hakimu Omar Mcha Hamza.
Ilionekana mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa alikuwa na ubishani kwa kila anachofahamishwa ,kuhusiana na vielelezo ambavyo vimefikishwa mbele ya mahkama, kwa ajili ya uthibitisho wa tuhuma ambazo zinamkabili juu yake  mahakamani hapo.
Awali, mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka, Seif Muhamed Khamis, aliiambia mahkama kuwa, shauri lililetwa mezani kwa ajili ya kusikilizwa na  ushahidi utatolewa  kwa upande wa upelelezi juu ya mtuhumiwa.
Shahidi wa upelelezi kutoka upande wa mahkama F 6368 D/C, Yussuf( 30), aliieleza mahkama kuwa  wakati akiwa katika kituo chake cha kazi Polisi Madungu, alipewa taarifa na Mkuu wake kuwa, kuna tukio la wizi wa Ng’ombe atoke na wenzake kwenda eneo husika kupata taarifa .
 
Alidai  walikwenda eneo la tukio, ambapo walimkuta raia  huyo, Suleiman Khamis, ambae alitoa taarifa za mwanzo, pamoja na mtuhumiwa akiwa na Ng’ombe, aliekusudia kumuuza bila ya kuhitaji shahidi, akidai kuwa ni wa familia na hahitaji itambue taarifa yoyote.
 

Aliendelea kudai  mahakamani hapo kuwa, walimchukua mtuhumiwa pamoja na Ng’ombe kumpeleka Kituoni , na mara baada ya kumuhoji alionekana kubadili majibu na kusema kuwa amemuokota mabondeni, hamjui mwenyewe wakati mwanzo alieleza ni wa familia.
                                   
Baada ya ushahidi huo Hakimu pia alimtaka mtuhumiwa kuthibitisha ushahidi wa hati ya maelezo ambayo aliyatoa mwenyewe wakati alipokuwa akichukuliwa maelezo katika mahkama ya mwanzo Chake chake, chini ya Hakimu, Thubeit na kuonekana kwamba alikiri kutenda kosa hilo.
 
“Muheshimiwa hakimu nina pingamizi na kielelezo kilichofikishwa mbele ya Mahkama yako, kwasababu mimi naaambiwa nimeiba wakati Ng’ombe kapewa mlalamikaji amtunze, hakuachwa Mahkamani usipokee kielelezo hicho” alidai mtuhumiwa.
 
Aidha alidai kuwa , yeye hata akioneshwa vielelezo vyote hafahamu chochote na kwamba hahitaji mashahidi wanaopokea taarifa za kusikia , hali ambayo ilionekana kusababisha upinzani mkubwa baina yake na hakimu mahkamani hapo.

“Kuletwa mbele ya mahkama kujibu tuhuma , haijulikani kwamba tayari wewe ni mfungwa wa kosa ,waache mashahidi wote waitwe wakimaliza,  mahkama itaangalia uwamuzi juu ya kuthibitika kwa kosa au laa ndio maana ya kuitwa mashahidi ,kwanini unaleta ushindani kwa kila unachofahamishwa” alisema Hakimu.
 
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, iliyowasilishwa mahkamani hapo, ilidai kuwa mnamo siku ya Aprili 16, 2012 majira ya saa 10:00 jioni mtuhumiwa aliiba Ng’ombe jike mwekundu mwenye thamani ya Tsh,300,000 maneo ya Mbuzini Chake chake   Pemba ,ambapo ni kosa kif, 267(1) na 274(1)(2)(C) sheria no.6/2004 sheria ya Zanzibar.
 
Nae, mwendesha mashtaka alimuomba Hakimu kupokea kielelezo cha maandishi ya maelezo ya mtuhumiwa iwe kama ni ushahidi utakaosaidia mahkama pamoja na picha ambazo, zilitolewa kueka kumbukumbu ya kukabidhiwa Ng’ombe, kwa ajili ya matunzo kwa mlalamikaji.
 
“Muheshimiwa hakimu ,shauri litaendelea kusikilizwa shahidi ambae ni Hakimu , aliyemchukulia maelezo kwa ajili ya ushahidi zaidi shahidi huyo leo hayupo hivyo naomba ipangiwe tarehe nyengine”aliema muendesha mashtaka.
 
Hakimu aliakhirisha shauri hilo hadi juni ,24 mwaka huu kwa kusikilizwa shahidi.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.