Habari za Punde

Sherehe za wauguzi zaingia dosari.

• Viongozi wa Wizara waingia mitini
Na Mwantanga Ame
KUKOSEKANA watendaji wa Wizara ya Afya katika sherehe za siku ya wauguzi, kumetia doa sherehe hizo hali iliyosababisha mgeni rasmi, mke wa Makamu wa Pili wa Rais, mama Asha Seif Iddi kukataa kusoma hotuba aliyoandaliwa na kuondoka.

Hali hiyo ilitokea muda mfupi baada ya mgeni rasmi kukagua maonesho yaliyoandaliwa na wauguzi na kupokea risala yao.

Na alipopewa nafasi ya kuzungumza,alisimama na kuanza kuhoji sababu ya kutokuwepo watendaji wa wizara ya afya wakati wao ndio waliomualika.

“Nashangazwa na viongozi wenu wao ndio walionialika na walijiorodhesha wote katika barua yao kuniomba niwe mgeni rasmi sasa nashangaa siwaoni hata mmoja,sasa na mimi hii hotuba siisomi,” alisema.

Alisema atakachokifanya ni kuirejesha hotuba hiyo kwa watendaji wa wizara hiyo.

“Mara nyingi wanaonekana wauguzi ndio wakorofi, lakini kumbe ni kinyume chake ni viongozi wenyewe ndio wakorofi,poleni sana nakuoneeni huruma,”alisema.

Hata hivyo, aliwataka wauguzi katovunjika moyo kutekeleza majukumu yao.

Mapema akisoma risala ya wauguzi, Asha Mkamba alisema kati ya wafanyakazi waliopo kwenye sekta ya afya asilimia 65 ni wauguzi ambao hutoa huduma za awali kwenye vituo vya afya na hospitali kuu.

Alisema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ni vyema serikali ikaona umuhimu wa kuwaandaa wauguzi kwenda na wakati katika kutoa huduma.

Alisema kazi kubwa ambayo serikali itahitaji kufanya ni kutoa nafasi za elimu kwa wauguzi ili waweze kufahamu mbinu mbadala za kuielimisha jamii namna ya kutumia kinga ili kuiwezesha kukabiliana na maradhi.

Alisema licha ya kuwepo mafanikio katika sekta hiyo,lakini bado kuna changamoto nyingi ikiwemo ya kushindwa kufikia kiwango cha kuzuia vifo vya watoto kulingana na viashiria vilivyowekwa kitaifa.

Alisema viashiria ambavyo wizara imeviweka ni kupunguza vifo hadi 130 kwa kila kinamama 100,000, kuzidisha idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya usimamizi wa wataalamu kufikia 90 kati ya wajawazito 100.

Alisema bado vifo vinavyotokana na uzazi ni vingi kwani kinamama 285 hufariki kati ya 100,000 wanaojifungua chini ya usimamizi wa wataalamu jambo ambalo linahitaji mkakati maalum kuhakikisha kila mtu anawajibika.

Alisema kada ya uuguzi inakabiliwa na tatizo la upungufu wa vifaa, upungufu wa wauguzi hali inayosababisha muuguzi mmoja huwahudumia wagonjwa 40 hadi 50 na maslahi duni.

Kauli mbiu ya siku ya wauguzi mwaka huu ni ziba mapengo katika kufikia malengo ya milenia.

2 comments:

  1. Viongozi waliona haya hana cha kuwaeleza wauguzi hakuna asijua mazingira magumu ya kiutendaji kazi hapa kwetu Zanzibar kun urasim, ubazirifu,uzembe,ugoigoi na kutowajibika ni mambo yanayo itesa Zanzibar .mke wamnene kaonamwenye mabosi wao wameingia mitini?

    ReplyDelete
  2. MIE NASHANGAZWA NA KITU KIMOJA TU NA HII NCHI YETU HAWA WAKE WA MARAIS KWANI NI WANA SIASA AU VIONGOZI WA SERIKALI MANAAKE UTAONA SIKU HIZI MAMA ASHA, MKE WA KIONGOZI GANI SIJUI AKEMEA KITU FULANI NA KILA KIKAO YUPO MBELE, INABIDI SERIKALI IANZE KUANGALIA HILI KWASABABU SIONI KAMA HAWA WANATAKIWA WAINGIE KATIKA MAMBO YA SERIKALI SANA

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.