Habari za Punde

Watuhumiwa wa bomu waongezeka

Na Joseph Ngilisho, Arusha

IDADI ya watuhumiwa wa tukio la kuripua kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi mkoani Arusha, imeongezeka hadi kufikia 12, kati yao majina tisa yametajwa na matatu bado ni siri kwa ajili ya uchunguzi.

Aidha jeshi la Polisi nchini kupitia Mkuu wa  Polisi,(IGP) Saidi Mwema, wametangaza donge nono la shilingi milioni 50 kwa mtu yoyote atakayefanikisha kufichua mtandao wa kigaidi nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa polisi Mkoani Arusha, Liberatus Sabasi, wakati akitoa taarifa juu ya hatua walizochukua tangu kutokea kwa mripuko wa bomu hilo Mei 5 mwaka huu, majira ya saa 4.30, ambapo watu watatu walifariki dunia na 66 kujeruhiwa.


Kamanda Sabasi aliwataja watuhumiwa tisa kuwa ni Victor Ambrose Kalisti (20) mkazi wa kwa Mromboo Arusha, Joseph Yusuph Lomayani (18),George Bathoromeo Silayo (23) mfanyabishara na mkazi wa Olasiti na Mohamed Sulemani Said (38) mkazi wa Ilala   Dar es Salaam ambae ndie mwenyeji wao aliyewafuata kwa gari binafsi uwanja wa ndege Dar es Salaam na kuwachukua hadi Arusha katika hoteli ya Aquline.

Wengine ni Said Abdallah Said (28), Said Mohsen na  Foud Saleem Ahmed (28)  raia wa Falme za Kiarabu, Abdulaziz Mubarak (30) raia wa  Saudi Arabia na  Jassini Mbarak (29) mkazi wa Bondeni Arusha.

Alisema kuwa watuhumiwa hao bado wanaendelea na mahojiano na tayari jalada la mashtaka yao limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya maamuzi ya kisheria.

Alisema katika hatua za awali zinaonesha bomu hilo siyo la kienyeji na pia wageni hao walikutwa na viza  halali ya kukaa nchini, kwa madai walikuja harusini. 

“Watuhumiwa hawa wa UAE tulipowahoji walidai wamekuja harusini, lakini tunaendelea nao,” alisema.

Aidha alisema ulinzi umeimarishwa katika kanisa lilikotokea mripuko huo.

2 comments:

  1. KWA KWELI NCHI IPO KTK WAKATI MGUMU!

    ReplyDelete
  2. Mcha mwana kulia mwisho humnyea nyimbo za kuashiria ugaid na siasa chafu zimezoeleka hapa Tanzania ya kitufika mtumlilie nani?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.