Na Othman Khamis,OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema wakati umefika kwa wananchi kuwa na hadhari katika kuangalia mtu mwenye muelekeo wa kuwafaa katika kuwasimamia kusukuma mbele maendeleo yao.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizindua rasmi jengo jipya na la kisasa la skuli ya msingi Miwani ndani ya jimbo la Uzini lililojengwa ndani ya kipindi cha miezi miwili na Mwakilishi wa Jimbo hilo, Mohammed Raza.
Balozi Seif alisema ile tabia ya baadhi ya wananchi kukumbatia watu wanaoendeleza ubinafsi inafaa kupigwa vita kwa hali yoyote ile kwa vile inachangia kuzorotesha kasi ya maendeleo ya wananachi.
Aliwahimiza viongozi, washirika na wahisani zikiwemo taasisi za kijamii na zile za maendeleo zilizomo katika halmashauri za wilaya kujikita zaidi katika kuunga mkono juhudi za wananachi kwenye sekta za maendeleo na kiuchumi wakiangalia zaidi ile sekta muhimu ya elimu.
Balozi Seif alimpongeza Mwakilishi wa jimbo hilo kwa hatua yake aliyochukua ya ujenzi wa jengo hilo la madarasa mawili lililokamilika huduma zote ikiwemo vikalio ambalo limesaidia kuiepusha skuli ya Miwani kuchukua wanafunzi katika mikondo miwili.
Alisema juhudi za Mwakilishi huyo ni miongoni mwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 ya CCM pamoja na kukamilisha ahadi alizotoa wakati wa kuomba ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo.
Aliwakumbusha viongozi wengine wa jimbo, wilaya na mkoa kuunga mkono jitihada za wananachi wa Miwani katika kukamilisha jengo jengine la madarasa sita la skuli hiyo ambalo linahitaji nguvu za ziada za viongozi hao.
Alisema katika kuunga mkono juhudi za wananchi anaahidi kuchangia shilingi milioni 2,000,000.
“ Sisi viongozi kuanzia Wawakilishi wa kuteuliwa, Mbunge, Madiwani na hata halmashauri za wilaya tunalazimika kuunga mkono juhudi hizi ili kutowavunja moyo wananchi tunaowaongoza katika majimbo yetu,” alisema.
Akitoa salamu za Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) iliyosaidia vikalio vyote vya jengo hilo vyenye thamani ya shilingi milioni 16,000,000, Msaidizi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Ame Haji Makame alisema benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi popote pale.
Alisema PBZ inajali maendeleo ya jamii na wakati mwengine kushawishika kusaidia miradi tofauti ikiwemo zaidi sekta ya elimu ambayo ndio mkombozi wa taifa lolote.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mwanaidi Saleh alimpongeza Mwakilishi wa jimbo la Uzini, kwa juhudi zake za kusaidia nguvu za wizara hiyo katika ukamilishaji wa majengo ya skuli.
Alisema juhudi za Mwakilishi huyo limeipunguzia mzigo mkubwa wizara ya elimu wa kukamilisha majengo kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na wizara hiyo.
Akitoa shukrani zake katika hafla hiyo,Raza alisema kwamba uwepo wa viongozi katika jamii upo kwa ajili ya kusimamia matakwa ya wananchi.
Alisema tabia ya baadhi ya viongozi kuigonganisha vichwa jamii ni kutowafanyia haki wanaowaongoza na hatimae inaviza maendeleo yao na kuwaongezea chuki na fitna baina yao.
Mapema katika risala yao iliyosomwa na Mwalimu wa skuli ya msingi ya Miwani, Juma Abdulla alisema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ndani ya kijiji hicho.
Jengo hilo limegharama za shilingi milioni 30,000,000.
No comments:
Post a Comment