Habari za Punde

Zanzibar ina ‘mateja’ 3000

Na Ameir Khalid,Ahmed Sakrani (OUT)

SERIKALI imesema Zanzibar ina watumiaji wa dawa za kulevya wapatao 3000.
 
Akijibu hoja za Wawakilishi katika ukumbi wa baraza hilo jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji, alisema juhudi za makusudi zinahitajika kuchukuliwa kuhakikisha Zanzibar inakuwa salama na dawa za kulevya.

Alisema dawa za kulevya ni janga na kwamba serikali iko tayari kupokea taarifa kutoka kwa mwananchi yeyote anaefahamu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Alisema serikali itatoa zawadi maalum kwa mtu huyo na taarifa zake zitakuwa siri kati yake na serikali.
Akizungumzia juu ya dawa ya kuulia kunguru iliyotumika kufanyia kazi hiyo alisema ni zaidi ya shilingi milioni 6.8 kwa ajili ya ununuzi wa sumu hiyo.

Kuhusu mradi wa nyumba ya wanaoacha dawa za kulevya, Waziri huyo alisema, serikali imo katika matayarisho ya kufanikisha mradi huo mwaka huu.

Mapema Wawakilishi walihoji fungu la ofisi ya faragha katika ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Tume ya Ukimwi, suala ambalo lilizua mjadala mkubwa.

Kwa mujibu wa kitabu cha wizara hiyo, ofisi ya faragha kwa mwaka wa fedha uliopita, iliomba kutumia shilingi 511,324,000 kwa matumizi kazi za kawaida, ambazo mgawanyo wake katika mishahara iliomba shilingi 211,324,000 na mambo mengineyo idara hiyo ilipanga kutumia shilingi 300,000,000.

Hata hivyo, fedha zilizoingizwa kutoka hazina kuu ya taifa, ni shilingi 403,324,000 ambapo kwa mishara ilikuwa ni shilingi 211,324,000 na mambo mengineyo ilitumia shilingi 192,000,000 ikiwa sawa na asilimia 79.

Kwa mwaka huu wa fedha kitengo hicho kimeombewa shilingi 515,150,000, ambazo zitatumika kwa ajili ya shughuli zote za ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa utoaji wa huduma na kuimarisha mazingira ya kazi katika kuleta ufanisi.

Lakini wajumbe hao walieleza kupata hofu na matumizi yaliopangwa ndani ya bajeti hiyo, kwa baadhi ya mafungu hasa ya ofisi ya faragha na ukimwi na Idara ya watu wenye ulemavu na kusema watahitaji kupewa maelezo ya kina ili waweze kuiachia bila ya kutoa shilingi zao.

Wawakilishi ambao walitishia kutoa shilingi ni pamoja na Ismail Jussa Ladhu wa Mji Mkongwe, Hija Hassan Hija wa Kiwani, Wadi Mussa Mtando wa Mkwajuni huku wengine wakitaka maelezo ya kina juu ya mafungu hayo.

Wajumbe hao walieleza kupatwa na wasiwasi juu ya makadirio yaliowekwa kwa mwaka huu kwenye kodi ya nyumba ya Makamu wa Kwanza wa Rais, kutoka shilingi milioni 24 hadi kufikia shilingi milioni 98 fedha ambazo walieleza ni kubwa na wametaka kupewa maelezo ya kina ya matumizi aya fedha hizo.

Aidha, wajumbe walionesha wasi wasi mwengine kwenye matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kitengo cha ukimwi ambacho kimeomba kupatiwa fedha za ziada kwa mwaka ujao wa fedha.

Tume hiyo kwa mwaka 2012/2013 iliomba shilingi 739,000,000, ambapo fedha za mishahara zilikuwa shilingi 238,162,000 na mambo mengineyo ilitengewa shilingi 500,838,000.

Hata hivyo, kitengo hicho hadi kufikia mwezi Mei 2013, kiliingiziwa shilingi 518,197,552 ambapo mishara ni shilingi 238,162,000 na mambo mengineyo ni shilingi 280,035,552 ikiwa ni sawa na asilimia 70 ya fedha hizo.

Fedha kutoka kwa wahisani kwa mujibu wa bajeti iliyopita,tume hiyo ilitarajia kupata shilingi 1,604,700,000, lakini hadi kipindi hicho walipatiwa shilingi 1,187,016,000 ikiwa ni sawa na asilimia 74.

Kwa mwaka ujao wa fedha kutengo hicho kimeomba baraza hilo, kuinidhishia idara hiyo shilingi 768,000,000 kwa kazi za kawaida, ambapo kati ya hizo shilingi 510,714,700, kwa ajili ya kuendeshea kazi na shilingi 257,285,300 za mishahara ya kitengo hicho kwa mwaka huo mpya wa fedha na fedha za maendeleo ni shilingi 50,000,000 kutokana na mchango wa serikali na wahisani ni shilingi 1,719,000,000.

Wajumbe hao wakifafanua wasi wasi wao huo walisema kwamba wanashangazwa kuona kitengo hicho kinaombewa fedha zaidi, wakati kikionesha kutopata mafanikio katika bajeti iliopita kwa vile kasi ya ugonjwa huo imepanda badala ya kupungua.

Walisema kupanda kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya maradhi hayo kwa upande wa Zanzibar kutoka asilimia 0.6 kwa takwimu za mwaka 2007 hadi kufikia asilimia moja hiyo ni hatari kubwa na inahitaji Tume iliopo kujiona imeshindwa kudhibiti kasi ya maradhi hayo.

Wengi wa wajumbe hao walisema kinachoonekana fedha nyingi zilizotengwa katika bajeti hiyo zilitumika kwa kuwanufaisha baadhi ya watu na sio malengo yaliowekwa katika bajeti hiyo kutokana mafungu yake kuonekana kwa kiasi kikubwa kutumika kwa elimu lakini hali bado ni ngumu tofauti na hapo nyuma.

Walisema wanapatwa na wasi wasi huo, baada ya huko nyuma kuwapo kwa taarifa kutoka kwa waathirika wa maradhi hayo kutokuwa na msaada wanaoupata kutoka ndani ya Tume ya Ukimwi.

Walisema inashanga kuona Tume hiyo imekuwa hodari ya kuandaa semina nyingi na warsha pamoja na makongamano lakini maradhi hayo ndio kwanza yameongezeka.

Kutokana na hali hiyo wengi wa wajumbe hao walisema hawatakuwa tayari kuipitisha bajeti hiyo hadi pale watakapopewa maelezo ya kina juu ya matumizi ya fedha hizo.

Baadhi ya wawakilishi wengine akiwemo wa Jimbo la Bububu, Hussen Ibrahim Makungu, alisema ipo haja ya kuona serikali inaandaa utaratibu wa kuwapatia malipo maalum watu wenye ulemavu kwa kuwa uwezo wao ni mdogo na hawawezi kufanya kazi.

1 comment:

  1. Watafika 300,000 hao...si tumeamua kuoneana aibu!

    Z'bar wala huhitaji fedha nyingi au utaalamu kuwajua wanaoingiza, kuuza unga au kula unga lkn. ndio hivyo tena....'watu wa kurehemewa'

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.