Na Said Ameir, Nanjing China
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia
watanzania wanaoishi katika Jimbo la Jiangsu nchini China kuwa hatima ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaamuliwa na wananchi wenyewe na si
vinginevyo.
Dk. Shein amesema mchakato wa
mabadiliko ya Katiba unaosimamiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba unaendelea
vyema na umefikia hatua nzuri ya uchambuzi wa maoni ya wananchi ambapo rasimu
ya maoni hayo yatawasilishwa kwenye mabaraza ya katiba kwa majadiliano zaidi.
Dk. Shein amesema hayo wakati
wa mkutano na watanzania ambao wengi wao wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu
vilivyoko katika Jimbo la Jiangsu uliofanyika katika hoteli ya Sofitel mjini
Nanjing jana katika siku yake ya pili ya ziara yake ya siku tatu katika jimbo
hilo.
“Tume imakamilisha awamu ya
kukusanya maoni ya wananchi na sasa iko katika hatua ya uchambuzi wa maoni hayo
ili kuandika rasimu ya kwanza ambayo nayo itapelekwa katika mabaraza ya Katiba
kujadiliwa” Dk. Shein alieleza.
Alifafanua kuwa mchakato huo
ni wa uwazi, hakuna uficho wa aina ye yote na unafanyika kwa kufuata njia za
kidemokrasia hali ambayo umepata sifa kutoka nje kwa kuwa nchi nyingine
zimeshindwa kufanya mabadiliko ya katiba zao kwa mfumo huo.
Dk. Shein amesema wananchi
hawapaswi kuwa na mashaka au kuleta sintofahamu katika jamii kwa kuwa kila mmoja
amepewa fursa ya kushiriki katika mchakato huo hatua kwa hatua hadi kufikia kupata katiba mpya kama
ilivyopangwa.
“Mchakato umewashirikisha
wananchi kutoka hatua ya kwanza ya kutoa maoni, mijadala katika mabaraza ya
katiba, Bunge na Baraza la Wawakilishi hadi kuipigia kura rasimu ya
mwisho”aliwaeleza wanafunzi hao.
Alifafanua kuwa rasimu ya
mwisho itakayopitishwa na Bunge itapigiwa kura kupitishwa kwake kunahitaji
kuungwa mkono na pande zote mbili za muungano.
Dk. Shein amewaambia
wanafunzi hao kuwa amefanya ziara nchini humu kwa lengo la kuimarisha uhusiano
kati ya Tanzania na China na kwamba hilo si jambo la bahati mbaya kwa sababu
ushirikiano huo ni muda mrefu.
“Nchi zetu zimekuwa na
ushirikiano kwa miaka mingi na sasa tumekuwa ndugu ambao tunasaidia kwa hali na
mali ”alisema na kuongeza kuwa Mpango wa Ushirikiano kati ya China na Afrika
ambao umepangiwa dola za kimarekani bilioni 20 Tanzania nayo itafaidika.
Rais wa Zanzibar amewaeleza
wananfunzi hao kuwa hali ya mipaka ya Tanzania ni salama na hakuna migogoro na
majirani na kuongeza kuwa hivi sasa mchakato wa utekelezaji wa ushirikiano
katika Jumuiya ya Afrika Masjhariki unaendelea vizuri.
“Haja ya viongozi waanzilishi
wa Bara la Afrika ni kutaka shirikisho la kisiasa Afrika lakini hilo ni vigumu
kulitekeleza lakini sisi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki lengo letu ni kuwa
na serikali moja ya shirikisho lakini ili kupata ufanisi mchakato wake
unakwenda hatua kwa hatua kufikia huko ” alifafanua.
Katika mkutano huo wanafunzi
walipendekeza wataalamu watanzania walioko nje washirikishwe katika mipango ya
serikali ya kubadilishana wataalamu katika nchi waliko kwa kuwa mara nyingine
wako wataalamu wageni wangependa kwenda Tanzania lakini hawajulikani au hakuna mtu wa
kuwasaidia kutimiza azma yao.
Hii ni mara ya pili kwa Dk.
Shein kukutana na watanzania wanaoko nchini wakati wa ziara yake inayoendelea
hivi sasa nchini humo. Mara ya kwanza alikutana na watanzania wanaoishi katika
jiji la Beijing.
No comments:
Post a Comment