Habari za Punde

AFYA YA AKILI YASISIMUA MAAFISA MIPANGOMIJI

Daktari bingwa mbobezi wa figo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka (kulia) akifafanua jambo wakati wa kikao kazi cha Maafisa Mipangomiji wa mikoa kinachofanyika mkoani Arusha.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Deogratias Kalimenze (Kulia) akiwa na wakurugenzi wasaidizi  akifuatilia uwasilishaji wa mada ya namna ya kulinda afya ya akili na umuhimu wa akili hisia katika maeneo ya kazi wakati wa kikao kazi cha Maafisa Mipangomiji wa mikoa kinachofanyika mkoani Arusha.
Maafisa Mipangomiji wa mikoa wakifuatilia uwasilishaji mada ya afya ya akili wakati wa kikao kazi cha Maafisa Mipangomiji wa mikoa kinachofanyika mkoani Arusha. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA

Maafisa Mipangomiji wanaoshiriki kikao kazi cha siku tatu mkoani Arusha wamejikuta katika msisimko wa hali ya juu kutokana na mada ya namna ya kulinda afya ya akili na umuhimu wa akili hisia katika maeneo ya kazi iliyowasilishwa wakati wa kikao hicho.

 

Mada hiyo iliyowasilishwa na daktari bingwa mbobezi wa figo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka ilikuwa sehemu ya mada zilizotolewa kwa Maafisa Mipangomiji kwenye kikao hicho lengo likiwa kuwapa ufahamu wa masuala tofauti na yale ya kitaaluma. 

 

Maafisa Mipangomiji hao wako katika kikao kazi ambapo jukumu kubwa la kikao hicho ni kuboresha utendaji kazi kwa wana taaluma hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

 

Akiwasilisha mada ya namna ya kulinda afya ya akili na umuhimu wa akili hisia katika maeneo ya kazi jana, Dkt Kweka amewaambia wana taaluma hao wa fani ya mipango miji kuwa, afya ya akili ni utimamu katika maeneo matatu aliyoyainisha kuwa, ni hisia, fikra na tabia.

 

Kwa mujibu wa Dkt Kweka, changamoto ya afya ya akili zimeongezeka sana duniani na kuathiri hisia, tabia, fikra na kusababisha mateso ya kimya kimya kwa mamilioni ya watu.

 

"Changamoto ya afya ya akili huathiri zaidi mawazo, hisia na tabia na hivyo kudhoofisha uwezo wa mtu kutekeleza majukumu ya kila siku" amesema Dkt Kweka.

 

Akigeukia upande wa akili hisia, Dkt Kweka amesema, hali hiyo inarejelea uwezo wa kutambua, kuelewa, kudhibiti na kutumia hisia kwa ufanisi.

 

"Viwango vya juu vya akili ya hisia vinahusishwa na afya bora ya akili, kwani watu walio na akili hisia kubwa wanao uwezo wa kukabiliana na mfadhaiko, mizozo na changamoto za maisha kwa ufanisi zaidi kuliko wasio na akili hisia". Amesema.

 

Mbali na mada hiyo ya namna ya kulinda afya ya akili na umuhimu wa akili hisia katika maeneo ya kazi Maofisa Miapangomiji pamoja na mambo mengine walipata fursa 

ya kujifunza Maadili, Muongozo wa Upangaji na Utekelezaji Mipango ya Uendelezaji Miji, Umuhimu wa Kufanya Ukaguzi wa Matumizi ya Ardhi pamoja na Uidhinishwaji Kazi za Mipangomiji kwenye Mfumo wa e-ardhi.


Kikao kazi cha Maafisa Mipangomiji wa mikoa kilichoandaliwa na idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kinatarajiwa kumalizika Sept 3, 2025 jijini Arusha.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.