Na Said Ameir, Nanjing China
Serikali ya Jimbo la Jiangsu
nchini China itajenga katika hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja kituo cha
uchunguzi wa magonjwa ya njia ya chakula na kitengo cha huduma kwa wagonjwa
wanaopata ajali katika hospitali ya Abdalla Mzee huko Pemba.
Mkurugenzi wa Idara ya
Ushirikiano wa Kimataifa katika Idara ya Afya ya Serikali ya jimbo hilo Bwana
Shi Zhiyu alieleza kuwa ujenzi wa vituo hivyo unatarajiwa kukamilika mwezi
Oktaba mwaka huu.
Bwana Shi ameeleza hayo
wakati alipokuwa akimkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipotembelea Hospitali ya Drum Tower mjini
Nanjing makamo makuu ya jimbo hilo.
Akiwa katika hospitali hiyo
Dk. Shein alitembelea vitengo mbalimbali na sehemu za kutolea huduma kwa
wagonjwa na pia alizungumza na madaktari wa kichina waliowahi kufanya kazi
Zanzibar.
“Tumefurahishwa na ujio wako
hapa. Tunajua upo hapa kuimarisha uhusiano wa China na Zanzibar. Umetimiza nia
yako ya kututembelea na hiyo inaonyesha jinsi unavyotuthamini ”alieleza Li.
Alibainisha kuwa hospitali
hiyo imekuwa ikitoa wataalamu wengi wanaokwenda kufanya kazi Zanzibar na timu
inayokwenda sasa ni ya 25.
“Kwa hakika ushirikiano wa
nchi yetu na nchi zinazoendelea katika sekta ya afya ulibuniwa tangu Uhuru hali
ya kuwa sisi wenyewe tulikuwa na hatujapiga hatua kubwa lakini tumeweza
kutekeleza kwa kuwa ilikuwa ni dhamira yetu” Li alisema.
Aliongeza kuwa maadhimisho ya
miaka 50 ya ushirikiano huo yatakayofanyika
mwaka ujao usiwe tu ni wa kuonyesha historia ya mafanikio yaliyopatikana
bali kujenga mustakabala nzuri wa ushirikiano wetu kwa miaka mingi ijayo.
“maadhimisho ya miaka 50 ya
Jiangsu kupeleka wataalamu wa afya Zanzibar tunayachukulia kama changamoto na
fursa kwetu kupanua ushirikiano huo” Li alisisitiza.
Ujenzi wa vituo hivyo
utaimarisha utoaji huduma za uchunguzi na tiba kwa wagonjwa wenye matatizo ya
njia ya chakula na kutaimarisha huduma kwa watu wanaoumia katika ajali.
Bwana Li aliongeza kuwa baada
ya kukamilika upanuzi wa hospitali ya Abdalla Mzee huko Pemba serikali ya jimbo
hilo litapeleka wataalamu zaidi kusaidia kutoa huduma katika hospitali hiyo.
Akizungumza baada ya mkutano
huo Dk. Ding Yibo ambaye alifanyakazi katika hospitali ya Abdalla Mzee huko
Pemba kati ya mwaka 1997 hadi 1999 alisema kuwa mara kwa mara wanapokutana na
watumishi wenzake wa kichina waliokuwa nao Pemba kuzungumzia jinsi walivyoishi
na kufanya kazi huko.
“Ni kipindi chenye kumbukumbu
nyingi katika utumishi wetu kila tunapokutana na wenzagu tuliofanya kazi pamoja
Pemba huzungumzia maisha yetu yalivyokuwa na kuwakumbuka marafiki zetu
huko”alieleza Dk. Ding.
Anasema sio siri kuwa kila
mmoja wao ana hamu kupata fursa ya kurudi tena kwa sababu walipokelewa na
kuishi vizuri na wenyeji wao na kuwa nao walirejesha upendo kwao kwa
kufanyakazi kwa bidii.
Wakati
huo huo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amekutana na Gavana wa Jimbo la Jiangsu Bwana Li Xueyong na kuzungumzia kuimarisha ushusiano
kati ya Zanzibar na Jimbo la Jiangsu.
Katika mazungumzo hayo Bwana
Li alisema mbali ya ushirikiano katika sekta ya afya sasa ni muda muafaka wa
kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Jimbo hilo na Zanzibar ikiwemo
sekta ya utalii.
Alipendekeza safari za
kitalii zinazofanywa na wananchi wa jimbo hilo nchini Tanzania zijumuishe pia
matembezi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa upande wake Dk. Shein
pamoja na kukubalina na pendekezo hilo amesema eneo jingine la ushirikiano ni
kwa makampuni ya kati ya jimbo hilo kuwekeza Zanzibar katika sekta mbalimbali
ikiwemo ya tekinolojia ya mawasiliano ya habari ikiwa ni njia ya kuingia katika
masoko ya Afrika.
Jimbo la Jiangsu lina
makampuni mengi yakiwemo makubwa ya eletroniki na tekinolojia ya habari na
mawasiliano.
No comments:
Post a Comment