Habari za Punde

Raza ajivua uenyekiti ‘Mapinduzi Cup’

Na Mwandishi Wetu
SIKU kadhaa baada ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kuelezewa kuwa yameanza, Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo Mohammed Raza, ameamua kujiondoa katika kamati hiyo.

Kwa mujibu wa barua yake ya Juni 25, 2013 yenye namba ya kumbukumbu PS/MPR/VOL.1/25/6/13 kwenda kwa mlezi wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi, Raza ametaja sababu kadhaa za kuchukua uamuzi huo.

Amesema ameomba apumzike baada ya kuisimamia kamati hiyo kwa heshima kubwa kwa miaka mitatu.
“Nimeamua kwa nia njema kabisa niweze kupumzishwa kuiongoza kamati hiyo, ili nami niweze kufanya mambo yangu mengine, na pia kulinda heshima yangu katika tasnia hii ya michezo”, ilisema sehemu ya barua hiyo.

“Kama unavyofahamu, nilipata heshima kubwa ya kuiongoza kamati ya mashindano ya Kombe la Mapimnduzi kwa vipindi vitatu, mwaka 2011 hadi 2013, kazi ambayo nimeifanya kwa kushirikiana na wenzangu kwa ufanisi mkubwa”, alisema Raza kumwambia Balozi Seif ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sherehe na Mapambo.

Hata hivyo, ameeleza kuwa, pamoja na uamuzi wake huo, ataendelea kutoa mashirikiano na makundi mbalimbali na wananchi wa Zanzibar katika kukuza michezo, endapo serikali itampa kazi nyengine yoyote.

Raza ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi jimbo la Uzini, amesisitiza kuwa, busara na hekima ndizo zilizomuelekeza kuchukua hatua hiyo.

Maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, yameanza, kwa mujibu wa baadhi ya wajumbe wa kamati ya mashindano hayo kumtembelea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, kumueleza hatua iliyokwisha kuanza.

Mwakani, Mapinduzi ya Zanzibar yanatimiza miaka ya 50, ambapo mashindano hayo yatashirikisha pia timu za Oman, Vietnam na China.

Jitihada za kumtafuta ili aeleze zaidi juu ya uamuzi wake huo, hazikuweza kufanikiwa, ikielezwa kuwa kwa sasa yuko nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.