Habari za Punde

Yanga kuifuata KCC Mwanza


Na Mwandishi Wetu
MSHAMBULIAJI nyota Tanzania, Mrisho Ngassa aliyerejea Yanga SC majira haya ya joto akitokea Simba SC, zote za Dar es Salaam, ataanza rasmi kuichezea timu hiyo Julai 6, mwaka huu mjini Mwanza.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara, watacheza na KCC ya Uganda badala ya Rayon Sport ya Rwanda Julai 6 na 7, mwaka huu katika sehemu ya ziara yake ya kulitembeza kombe lake la ubingwa wa ligi kuu mikoa ya kanda ya Ziwa, ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

TBL imekuwa ikiidhamini Yanga kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager tangu mwaka 2008 sawa na wapinzani wao wa jadi, Simba na ndiyo wamedhamini ziara hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga Baraka Kizuguto, amesema timu itaondoka Julai 5 Dar es Salaam, siku mbili tu baada ya kuanza mazoezi uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, kuelekea Mwanza.

Kizuguto amesema mechi ya kwanza itapigwa uwanja wa CCM Kirumba Julai 6, na ya pili itachezwa Julai 7, kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na baada ya hapo, mabingwa hao mara tano wa Kombe la Kagame, wataelekea mjini Tabora, kucheza mechi nyengine na wenyeji, Rhino FC waliopanda ligi kuu msimu huu Julai 11, mwaka huu uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.

Katika ziara hizo, Yanga watatembeza kombe lao la ubingwa wa ligi kuu, walilolitwaa kwa mara ya 24 msimu huu kwenye mitaa mbalimbali kushangiria na mashabiki wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.